GH Foundation yatoa mafunzo ukatili wa kijinsia.

TAASISI ya GH Foundation imefanya warsha ya kuwajengea uwezo askari wa Jeshi la Polisi, maofisa ustawi wa jamii, Waandishi wa habari na viongozi wa dini kupambna na ukatili wa kijinsia.
GH Foundation ilifanya warsha hiyo wiki iliyopita katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam ikiwa na lengo la kuboresha mifumo na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa kupambana na ukatili wa kijinsia.
Ililenga kuongeza ufanisi katika kushughulikia vitendo vya ukatili kwa kuwajengea uwezo maofisa wa polisi, maofisa wa ustawi wa jamii, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyombo vya habari katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Warsha hiyo ni sehemu ya jitihada za taasisi ya GH Foundation kutekeleza afua zake mbili ambazo ni kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na kupambana na ukatili wa kijinsia ili kukuza usawa na ujumuishaji katika kijamii.