ADDIS ABABA, Ethiopia –Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema Afrika inastahili kupata uwakilishi wake wa haki katika taasisi za kimataifa, ikiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Akihutubia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Guterres amesema ataendelea kushirikiana na AU kuhakikisha nia hiyo inafanikiwa.
“Africa iliachwa nyuma wakati wa kuundwa kwa mfumo huu wa kimataifa, na dhuluma zimeendelea kwa muda mrefu,” alisema Guterres. Alitoa wito wa kutolewa kwa viti viwili vya kudumu kwa nchi za Afrika katika Baraza la Usalama, akisisitiza kwamba hakuna kisingizio cha Afrika kuendelea kukosa uwakilishi wa kudumu katika karne ya 21.
Guterres aliahidi kuendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na nchi wanachama wake kuhakikisha kuwa mahitaji ya Afrika yanatimizwa na sauti ya bara hilo inasikika katika jukwaa la kimataifa.
Katika hatua nyingine, Guterres amesema kuna haja ya kufanya mageuzi muhimu ya kifedha kimataifa, akieleza kwamba nchi za Afrika mara nyingi hulipa gharama kubwa zaidi za mikopo ikilinganishwa na mataifa yaliyoendelea, jambo linalochelewesha uwezo wao wa kuendesha maendeleo yao wenyewe.
“Mataifa ya Afrika mara nyingi hulipa hadi mara nane zaidi katika riba za mikopo ikilinganishwa na nchi zilizoendelea,” amesema.
Guterres ataka madini Afrika yawanufaishe waafrika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa viongozi wa Afrika kuhakikisha kuwa rasilimali na madini ya thamani yaliyopo Afrika yanawanufaisha waafrika.
Akihutubia Mkutano wa Kawaida wa 38 wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, Guterres amewaomba viongozi hao kuhakikisha kuna haki katika usimamizi wa maliasili za Afrika, ambazo ni muhimu hasa upatikanaji wa nishati duniani.
Amesisitiza ukweli kwamba madini muhimu barani Afrika, kama vile cobalt na lithiamu, yanawezesha teknolojia ya kijani kibichi lakini kwa kiasi kikubwa yanatumiwa na makampuni ya kigeni.
Alihimiza kuwepo na mfumo wa haki unaohakikisha nchi za Afrika zinanufaika na utajiri wao wa madini, ambao unaweza kusaidia kukabiliana na changamoto za kimaendeleo.
PIA SOMA: Mkutano wa Umoja wa Afrika waanza Addis Ababa, Ethiopia
“Rasilimali za Afrika zinapaswa kuwahudumia watu wa Afrika,” Guterres amesema.
Katika hatua nyingine Guterres amezungumzia mzozo wa hali ya hewa, akibainisha kwamba wakati Afrika inachangia kwa uchache zaidi katika utoaji wa hewa chafu duniani, bara linaathirika zaidi na majanga yanayohusiana na hali ya hewa.
“Kunahaja ya mshikamano wa kimataifa ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo yanaathiri vibaya Afrika,” alisema. Nakutoa wito kwa mataifa tajiri kuongeza kiwango cha michango yao ili kusaidia mataifa ya Afrika kukabiliana na athari za hali ya hewa.
“Jumuiya za kimataifa lazima ziwajibike kwa pamoja ili kukabiliana na ukosefu huo wa usawa, hasa wakati Afrika ikiendelea kukabiliwa na changamoto kubwa zinazohusiana na hali ya hewa,” amesisitiza.
What’s up, I want to subscribe for this blog to obtain latest updates,
so where can i do it please help out.