Haki elimu yaweka mkazo elimu ya kujitegemea

TAASISI ya HakiElimu imetoa wito kwa serikali na wadau mbalimbali kuweka mkazo kwenye elimu ya kujitegemea ili kusaidia kukabiliana na changamoto za ushindani mkubwa wa soko la ajira katika dunia ya sasa.

Taasisi hiyo imesema elimu ya kujitegemea inapaswa kusisitizwa kama nyenzo muhimu kwa wahitimu wa vyuo na shule inayoweza kuwasaidi kutumia fursa zilizopo kujikwamua kiuchumi.

Mkuu wa Programu wa HakiElimu, Godfrey Boniventure, amesema elimu hiyo ni muhimu katika zama za sasa ambapo ushindani wa soko la ajira ni mkubwa na wahitimu wanazidi kuwa wengi katika jamii kutokana na kuongezeka kwa fursa za watanzania kupata elimu.

Advertisement

Aliyasema hayo kwenye kongamano maalum lililofanyika kwa uratibu wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kwa kushirikiana na Chuo cha VIA cha Denmark, chuoni hapo na kuwaleta wataalamu wa elimu kutoka nchi mbalimbali kujadili namna elimu ya kujitegemea inavyoweza kuboresha maisha ya wahitimu.

SOMA: Hakielimu yagusa changamoto za elimu nchini.

Boniventure alisisitiza kuwa maboresho katika sekta ya elimu, ikiwemo uimarishaji wa miundombinu na marekebisho ya sera, ni muhimu sana yakaambatana na juhudi za kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi wa kujitegemea.

Alisema uwezo wa kuanzisha biashara, kutumia teknolojia, na kutatua changamoto za kijamii ni baadhi ya nguzo katika elimu ya kujitegemea, hasa katika muktadha wa ushindani wa soko la ajira na mazingira yanayobadilika kila mara.

Kuhusu biashara alisema elimu ya kujitegemea inawapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa ujasiriamali unaowawezesha wahitimu kutambua fursa za kiuchumi, kubuni bidhaa au huduma, na kuanzisha biashara ambazo zinaweza kuwapatia kipato cha kudumu.

“Hii ni muhimu katika mazingira haya ambayo ajira rasmi ni chache, kwani wahitimu wanakuwa na uwezo wa kujiajiri. Wanajifunza namna ya kusimamia biashara zao, kuandaa mipango ya biashara, kutafuta mitaji, na jinsi ya kudhibiti hatari za kibiashara,” alisema.

Kuhusu Teknolojia alisema ni msingi wa maendeleo ya kisasa, na elimu ya kujitegemea inawapa wahitimu uwezo wa kutumia teknolojia kwa njia ya ubunifu ili kuendesha shughuli zao.

“Wahitimu wanajifunza kutumia zana za kidigitali kama vile kompyuta, simu za mkononi, na mtandao wa intaneti kwa kuendesha biashara zao, kutangaza bidhaa, na kuwafikia wateja,” alisema.

Alisema matumizi ya teknolojia pia yanaongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara huku akitoa mfano kwamba wajasiriamali wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kufanya masoko kwa gharama nafuu, au kutumia programu za kompyuta kufuatilia hesabu za biashara na hivyo kuwapa uwezo wa kushindana katika soko la ndani na hata la kimataifa.

Kuhusu kutatua changamoto za kijamii alisema elimu ya kujitegemea inawajengea wahitimu uwezo wa kubaini matatizo yaliyopo katika jamii na kutafuta suluhisho kupitia miradi ya ubunifu.

SOMA: HakiElimu yataka adhabu chanya mashuleni

Alisema wahitimu wanaweza kuona changamoto kama fursa za ubunifu na ujasiriamali, kama vile ukosefu wa huduma fulani au tatizo la mazingira.

Akitoa mfano alisema kijana anaweza kuanzisha biashara ya kuchakata taka ili kusaidia kuondoa taka za plastiki katika jamii yake, huku akipata kipato.

“Kwahiyo katika dunia ya sasa, ambapo fursa za ajira rasmi zinapungua, elimu inayompa mwanafunzi uwezo wa kujiajiri au kutoa huduma inayohitajika na jamii ni muhimu zaidi. HakiElimu inaamini kuwa mtoto wa Kitanzania anayepata elimu bora atakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii,” alisema.

Alipokuwa akifungua kongamano hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Willison Mahera, alisema elimu ya kujitegemea inaendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023.

Alisema Sera hiyo inaweka mkazo kwenye ubora wa elimu na ushirikiano wa jamii katika kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea.

Alisema kwa zama hizi za kidigitali na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia, ujuzi wa kujitegemea unasaidia si tu katika kujiendesha kimaisha, bali pia katika kuleta uvumbuzi na maendeleo endelevu.

Alisema wahitimu wanaozalishwa na mfumo wa elimu wenye mkazo kwenye kujitegemea wanakuwa na nafasi nzuri ya kubuni fursa mpya, kuanzisha miradi ya kiuchumi, na kujiajiri wenyewe, hali inayosaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

Kongamano hilo la siku mbili lilijadili pia masuala ya elimu jumuishi, teknolojia, masuala ya kijinsia, ujuzi wa ubunifu, na elimu ya sayansi, ambayo ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya kujitegemea kwa wahitimu na kwa taifa kwa ujumla.