SHIRIKA la HakiElimu limependekeza kuwa na adhabu chanya mashuleni ili kuwaepusha wanafunzi na majanga ikiwemo vifo ambavyo usababishwa na adhabu kali zinazotolewa na walimu.
Pia inapendekeza dhana ya dhabu chanya kupewa mkazo katika mafunzo tarajali na kazini kwa walimu ili kuwasaidia kuepukana na matumizi ya adhabu za kikatili.
Akizungumza leo Machi 22, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk John Kalage amesema kwa mfano wakati wa mafunzo kwa vitendo kwa walimu utoaji adhabu unaweza kuwa moja ya eneo la tathmini.
HakiElimu imetoa mapendekezo hayo ikiwa ni siku tano tangu mwanafunzi wa kidato cha kwanza Gloria Faustine (14) wa shule ya sekondari Mwinuko Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kuangukiwa na jiwe na kusababisha kifo chake wakati akichimba kifusi kama sehemu ya utekelezaji wa adhabu baada ya kutumia lugha ya Kiswahili shuleni kinyume na taratibu za shule hiyo.
Mbali na Gloria kupoteza Maisha mwanafunzi mwingine Emmanuel Lyatuu alijeruhuiwa na amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture akiendelea kupatiwa matibabu
Dk Kalage amesema pamoja na utaratibu uliowekwa na mamlaka juu ya utoaji adhabu kwa Watoto ili kulinda usalama na uhai wao, matukio kama ya adhabu zinazoleta matokeo hasi yanazidi kuongezeka na kuibua hofu kwa wazazi na wanafunzi kwani shule sio salama sana kwa watoto.
“Tunatambua walimu wana jukumu la kuwafundisha na kuwajenga wanafunzi katika mwenendo unaofaa, hata hivyo jukumu hili wanaweza kulitekeleza kwa kutumia mbinu mbali mbali ikiwemo utoaji adhabu chanya ambazo zitamsaidia kufikia malengo ya utoaji wa adhabu.
“Badala ya kumwambia akachimbe vifusi mpe adhabu ya kuandika Insha kwa kingereza, kusoma vitabu vingi vya kingereza, wape midahalo ya kingereza, mazoezi ya mara kwa mara, adhabu hii ingewasaidia zaidi wanafunzi kujifunza lugha hiyo kuliko adhabu iliyotolewa.”Amesema
Amesema kuwaadhibu wanafunzi kwa sababu za kitaaluma kama vile kushindwa kuzungumza Kingereza, kuandika au kukokotoa kwenye hisabati hakuwezi kutatuliwa kwa kumpa mwanafunzi adhabu ambayo haimwelekelezi katika kujifunza kile anachotakiwa.
Dk Kalage amesema huwezi kuimarisha ujifunzaji wa lugha ya pili kwa kuzuia matumizi ya lugha mama.
“Shule nyingi za sekondari kuna kanuni inayosema speak English only, no English no service, hii inatengeneza ombwe kubwa katika ujifunzaji na ufundishaji wa kingereza au lugha yoyote.
Nae, Mkuu wa Miradi HakiElimu Godfrey Boniventura amesema moja ya malengo ya elimu kama yaliyobainishwa kwenye mtaala wa sekondari wa mwaka 2005 toleo la 2013 ni kuwawezesha wanfunzi kuwasiliana kwa ufasaha kwa lugha ya Kiswahili.
Pia sera ya elimu ya m waka 2014 inaweka wazi kuwa serikali itahakikisha kuwa lugha ya Kiswahili, Kingereza na nyingine za kigeni zinafundishwa kwa ufashaa na ufanisi katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
“Ni wazi kuwa Watoto wanaotoka shule za msingi na hasa za umma kuingia kidato cha kwanza wanakuwa hawajawa tayari kuweza kutumia lugha ya Kingereza katika kuzngumza na kujifunzia.
Kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari, itatoa fursa kwa watoto kujfunza kwa ufasaha na kufundishwa vema Kingereza na lugha nyingine kama lugha za kigeni..
.