DODOMA; Hakuna zuio lolote la kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za polisi kwenye vituo vilivyo nje na maeneo yao, Bunge limeelezwa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa wa Magomeni, Mwanakhamis Kassim Said, aliyetaka kujua kwa nini Jeshi la Polisi haliondoi zuio la kuwahudumia wananchi wanaokwenda kupata huduma kwenye vituo nje ya maeneo yao.
“Kwa mujibu wa kifungu namba 7 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022, kikisomwa pamoja na Kanuni za Jeshi la Polisi (PGO) Namba 309.
“Mtu yeyote aliyetendewa au anayefahamu jinsi kosa lilivyotendeka au linavyotaka kutendeka anatakiwa kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi kilichokaribu na taarifa hiyo itachukuliwa na kufanyiwa kazi.
“Hivyo, hakuna zuio lolote la kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za polisi kwenye vituo vilivyo nje na maeneo yao,” amesema Naibu Waziri.