SUDAN: Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Christou Christou amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu yanapaswa kurudi na kuwasaidia watu wa Sudan.
Wito huo umekuja baada ya mashirika mengi ya kimataifa ya misaada kusitisha kupeleka huduma za kibinadamu nchini Sudan.
SOMA: Jeshi lakubali kusimamisha vita Sudan
“Katika kipindi hiki cha miezi 15 ya vita nchini Sudan,mtu mmoja kati ya watatu waliojeruhiwa ni mwanamke au mtoto wa chini ya umri wa miaka 10, mashirika mengi yameamua kunyamaza,” Christou amesema na kuongeza:
“Tangu wiki iliyopita wajumbe hao wa pande mbili zinazovutana wako Geneva kuzungumza mjumbe wa Umoja wa Mataifa, lakini hakuna kilichofanyika,”amesisitiza Christou.
Hatahivyo amesema MSF itaendelea kuzungumza na pande zote mbili zinazovutana, ili kupata misaada ya kibinadamu kwa ajili ya mamilioni ya Wasudan wanaohitaji misaada ya dharura ya kibinadamu kama vile chakula ,maji na makazi.
Kwa sasa Sudan inakabiliwa na tatizo la ukame ambao wengi wameachwa bila ya makazi, huku wengine wakiripotiwa kushindwa kujikimu kimaisha, kwani wameishiwa fedha, chakula na njia karibu zote za kujipatia riziki.
Mashirika mengi ya kutoa misaada yamesitisha shughuli zao kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi wake kushambuliwa kwa vituo vyao, kuporwa kwa misaada, kunyimwa ruhusa ya kufikia maeneo yanayohitaji misaada na kutopata ufadhili wa kutosha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Mataifa umezishutumu pande zote mbili zinazopigana, Jeshi la Sudan na kikosi maalumu cha wanamgambo RSF kwa kuzuia misaada kufikishwa kwa watu walengwa na kukiuka haki za binadamu.
“Kwa mfano katika mji wa El Fasher,vituo vya MSF vimeshambuliwa mara tisa tangu Mei 19 na karibu kila kona ya Sudan,wahudumu wa afya wanatishwa, wagonjwa wanauawa na vituo vya afya vinalipuliwa kwa mabomu,” amesema Christou.
Mzozo wa Sudan umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha takribani watu milioni 11 bila ya makazi, zaidi ya nusu ya Wasudan hawana chakula cha kutosha na hali inabashiriwa itazidi kuwa mbaya.
Chanzo: BBC