Harakisheni umilikishwaji ardhi – Mavunde

MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amewataka wataalamu wa Ofisi ya Idara ya Mipango Miji Jiji la Dodoma kuharakisha zoezi la umilikishwaji ardhi kwa wananchi wa Mtaa wa Ndachi kata ya Mnadani ili kupunguza migogoro ya ardhi katika eneo hilo.

Mavunde ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika kata ya Mnadani eneo la Ndachi katika Mkutano uliosimamiwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde Charles Mamba na kuhudhuriwa na wataalamu wa Ardhi Jiji,DUWASA na TANESCO.

“Nampongeza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Jabir Shekimweri kwa hatua za awali za kuvunja kamati ya ardhi na kuelekeza zoezi la umilikishwaji wa ardhi lifanyike kupitia ubalozi wa eneo husika.

Niwatake wataalamu wa Jiji kutochelewa kutekeleza maelekezo haya na kuhakikisha tunaanza zoezi hili la umilikishaji ardhi kwa uharaka kupitia balozi hatua ambayo itasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Zoezi hili likikamilika litaenda sambamba na ufunguaji wa barabara za mitaa ili kuruhusu shughuli zingine za maendeleo kufanyika.

“Lakini pia nataka kuwapa taarifa kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja,Serikali chini ya uongozi wa Mh Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itatekeleza ujenzi wa kituo cha Afya kikubwa katika kata ya Mnadani ikiwa ni pamoja na kuanzisha ujenzi wa shule ya Msingi mpya ya Matuli kwa ushirikiano wenu ninyi wananchi na mimi Mbunge wenu”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali, Diwani wa kata ya Mnadani Mh.Paulo Bankiye amewataka wananchi wote kutoa ushirikiano wakati wote wa  zoezi hilo la umilikishaji likiendelea.

Akitoa maelekezo,Mwenyekiti wa CCM Wilaya Cde. Charles Mamba amewataka viongozi wote wa kuchaguliwa wa serikali kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi na kutatua kero zao za msingi kwa wakati na kueleza Taasisi zote za serikali kupeleka huduma za msingi za kijamii kwa wananchi pindi zoezi la umilikishaji ardhi litakapokamilika.

Habari Zifananazo

Back to top button