Hatma Wabunge Viti Maalumu mikononi mwa Tume

SHERIA ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 imeweka mwongozo wa namna ya kupata wabunge wa viti maalumu.
Bunge la 12 lilikuwa na wabunge 113 wa viti maalumu wakiwemo 94 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kifungu cha 112 (1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 kimeeleza kutakuwa na wabunge wanawake wa viti maalumu katika Bunge kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 66 ya Katiba.
“Chama cha siasa kinachogombea katika uchaguzi wa wabunge utakaofanyika baada ya kuvunjwa kwa Bunge kinaweza kupendekeza na kuwasilisha kwa Tume (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi) majina ya wagombea wanawake wenye sifa kwa ajili ya uteuzi wa viti maalumu vya wanawake si chini ya siku thelathini kabla ya siku ya uchaguzi,” imeeleza sheria.
Imeeleza Tume itaainisha idadi ya wagombea wanawake watakaoteuliwa na kila chama cha siasa na majina ya wagombea waliopendekezwa kwa Tume yatakuwa katika mpangilio kwa kuzingatia kipaumbele.
“Kila mwanamke mgombea aliyependekezwa kwa Tume atatakiwa kujaza fomu ya uteuzi. Masharti ya Ibara ya 67 ya Katiba yatatumika kwa kila mwanamke ambaye amedhaminiwa na chama cha siasa,” imeeleza sheria.
Imeongeza: “Kwa kuzingatia Ibara ya 66, 67 na 78 za Katiba na kwa mujibu wa mpangilio wa kipaumbele uliooneshwa katika orodha iliyopendekezwa na kila chama cha siasa, Tume itateua na kutangaza idadi ya wanawake wagombea kutoka katika vyama vya siasa vinavyohusika kuwa wabunge wanawake viti maalumu”.
Sheria imeeleza Tume itatuma taarifa ya uteuzi kwa Spika wa Bunge na kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa vinavyohusika.
“Orodha ya majina ya wanawake wagombea waliopendekezwa kwa Tume kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba na kila chama cha siasa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, kwa kuzingatia Ibara ya 76(3) ya Katiba itakuwa ndiyo orodha itakayotumiwa na Tume kwa madhumuni ya kujaza nafasi wazi ya ofisi ya mbunge wa viti maalumu vya wanawake wakati wa kipindi chote cha uhai wa Bunge,” imeeleza sheria.
Imeongeza: “Isipokuwa kwamba inapotokea orodha ya majina iliyowasilishwa kwa Tume imemalizika, Tume itakitaka chama husika kuwasilisha orodha ya nyongeza ya majina ya wagombea wanawake viti maalumu wanaopendekezwa kwa ajili ya uteuzi”.



