Hausigeli’ aliyemkata shingo mtoto akamatwa

DAR-ES-SALAAM: JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemkamata msichana aliyemjeruhi mtoto kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni.

Julai 17, mwaka huu taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ilieleza kuwa dada huyo wa kazi za nyumbani, Clemensia Mirembe (19) alimjeruhi Malick Hashim (6) Julai 15, mwaka huu saa 12 jioni Goba Kinzudi, Kinondoni.

SOMA: Samia kugharamia tiba mtoto aliyenusurika kuchinjwa

Advertisement

Kamanda Muliro amesema jana kuwa msichana huyo alikamatwa Julai 21, saa 4:00 usiku akiwa amejificha kwenye pagala Goba Kinzudi. Baba wa Malick, Hashim Mohammed alisema Malick ndiye aliyemtaja binti huyo mama yake alipomuuliza ni nani alimjeruhi.

Inadaiwa Clemensia ni mkazi wa Kasulu mkoani Kigoma na amefanya kazi kwenye familia ya Mohammed kwa miezi saba. Mtoto huyo anatibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikwenda hospitalini hapo juzi na alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atalipia gharama zote za matibabu kwa mtoto huyo.

Mtoto huyo alipata majeraha yaliyotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti hivyo kusababisha ashindwe kupumua, kuzungumza, anapata maumivu na amepoteza damu nyingi sana.

Wataalamu MNH wamemfanyia upasuaji mkubwa uliochukua saa nne ili kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi yaliyopata changamoto kwenye shingo na kutibu jeraha la nyuma ya shingo. Jeraha la mbele ya shingo liliharibu tezi la mbele kwa kulikata katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi.

Pia mtoto huyo anapata maumivu makali kutokana na jeraha alilokatwa mbele ya shingo ambako hewa inayotoka kwenye mapafu hupita ili iende kwenye sanduku la sauti kumwezesha kuhema na kuzungumza kwa mantiki.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeshauri wazazi, walezi, walimu na jamii wa ujumla wawafundishe watoto wajenge tabia ya kutembea katika makundi na pia wasikubali kuwa karibu na watu wasiowafahamu.

“Watoto wasitumwe maeneo ambayo kwa mazingira ni hatarishi ikiwa ni pamoja na kuacha kuwatuma watoto wadogo maeneo mbalimbali nyakati za usiku,” alisema Kamanda Muliro.