Heko sekretarieti EAC kwa mipango thabiti

WIKI iliyopita kulikuwa na vikao takribani vitatu jijini Arusha vilivyohusu masuala ya maendeleo kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika vikao hivyo baraza la 40 la dharura kuhusu sekta ya biasahara, viwanda, fedha na uwekezaji lilikutana kujadili mambo mbalimbali lakini jambo kubwa likiwa ukuaji wa viwanda.

Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi kutoka nchi za EAC na kujadili masuala muhimu ya uendelezaji wa viwanda kwa lengo la kuhimiza ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kikanda ndani ya Jumuiya hiyo.

Baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni maendeleo kuhusu utekelezaji wa mkakati wa bidhaa za ngozi na viatu, utekelezaji wa mkakati wa pamba, nguo na mavazi.

Mengine ni utekelezaji wa mpango wa hatua ya sekta ya magari na maendeleo ya mpango wa ukanda wa EAC katika sekta ya dawa 2017-2027.

Kwa mujibu wa taarifa ya sekretarieti ya EAC, jumuiya hiyo inaendelea kujitolea kukuza uchumi wa kikanda ulio shirikishi, unaosaidia ukuaji wa viwanda endelevu na kuboresha maisha ya wananchi wake.

Mkutano huo pia ulijadili Sera na Muswada wa EAC dhidi ya bidhaa bandia.

Mambo mengine yaliyojadiliwa humo ni mashauriano ya awali kwa mawaziri wa fedha, taarifa kuhusu mapitio ya sheria ya EAC ya kuondoa vizuizi visivyo vya kodi ya mwaka 2017 na ukamilishaji wa kanuni.

Mengine yaliyojadiliwa ni uendelezaji wa kanuni za eneo huru la fordha la EAC, ripoti ya maendeleo kuhusu utekelezaji wa mkakato wa EAC wa kukuza mazao ya nje.

Tunaipongeza sekretarieti kwa kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na kufanya majadiliano yakiwemo yaliyofanyika hivi karibuni kwani tunaamini yataleta tija kubwa kwa nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati.

Tunaamini changamoto zinazojitokeza katika jumuiya hiyo zimekuwa zikijadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi na zitaendelea kutatuliwa kwa manufaa ya serikali na wananchi wa EAC.

Ni wazi suala la bidhaa bandia limekuwa sugu miongoni mwa nchi hizi, hivyo tunaamini mijadala katika mikutano hiyo itazaa matunda na hili tatizo kugeuka historia.

Kama tunavyofahamu, kuna soko la pamoja la Afrika Mashariki ambalo tunaamini ni mkombozi kwa wanajumuiya, wafanyabiashara na wanunuzi kutokana na sheria na kanuni juu ya uuzwaji wa bidhaa zenye ubora kwenye soko hilo.

Ni matarajio ya kila mwana EAC kuona jumuiya inapiga hatua kwenye nyanja mbalimbali kukuza uchumi na tunaamini hilo linawezekana kwa nguvu ya pamoja ya viongozi na wananchi.

Tunaamini huu ni wakati mwafaka kwa wanajumuiya kuwekeza zaidi kwenye viwanda, bidhaa bora na kilimo ili kuipandisha EAC.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button