ZANZIBAR; RAIS wa klabu ya Yanga, Hersi Said amesema hakupenda kuona fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na Yanga ifike hatua ya penalti, kwa sababu hawana bahati na hatua hiyo.
Akizungumza na Daily News Digital, Hersi amesema hakupenda kufikia hatua ya kupiga mikwaju ya penalti kwa sababu ya kumbukumbu za kupoteza michezo miwili.
“Nilitamani mpira umalizike ndani ya dakika 90, kwa kuwa michezo miwili tumeondolewa katika hatua ya penalti, Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mamelodi Sundowns,” amesema Hersi.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/yanga-mwendo-wa-ubingwa-tu/
Amesema kulingana na ubora wa Azam FC waliouonesha kwa msimu huu, hawakutaka kufika hatua ya kupiga mikwaju ya penalti na alitamani mechi itamatike ndani ya dakika 90.
“Tumecheza fainali nyingi lakini hii ina ubora mkubwa na kutokana na ubora wa timu zote mbili, Azam FC walikuwa bora sana, lakini kama ninavyosema suala la penalti halina mwenyewe.
“Nimpongeze sana kipa wa Azam FC (Mohammed Mustafa), alikuwa bora sana hasa kuokoa mipira mingi ya hatari, lakini Diarra (Djigui) naye amefanya kazi kubwa hasa kucheza penalti ya tano ya Azam,” anasema Hersi.