Heshima ni muhimu katika kudai haki, kutoa ushauri

Nikiwa Mtanzania na mtaaluma mzamivu wa maendeleo ya binadamu na afya bora ya akili, nimewiwa tukumbushane kuhusu kudai haki, kuheshimiana na kutoa ushauri kuhusu maendeleo yetu endelevu.
Hatua za maendeleo tulizopiga tangu uhuru ni kubwa, hivyo ni muhimu tuzidi kusonga mbele bila kuruhusu hali yoyote itakayoturudisha nyuma hususani kutugawa au kusababisha mfarakano na kubomoa heshima, uhuru, umoja na amani ambayo ni ngao za taifa letu.
Nianze kwa kutuma salamu za pole kwa wote ambao ama wao wenyewe, au ndugu zao wamejeruhiwa, au wameuawa kwa kudai haki. Pamoja na kuzikubali na kuzithibitisha sheria na itifaki mtambuka za kimataifa, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani ni nchi ya kipekee, huru na inayojitawala.
Hivyo, haiwezi kulazimishwa kufanana na nchi nyingine yoyote na wala haina mbadala wake. Ni nchi huru yenye mazingira na tamaduni zake inayojiongoza kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu zake. Katika hali ya upekee wa kila nchi; masuala ya ulinzi, usalama, utoaji haki na ustawi wa jamii ni majukumu ya kila serikali na watu wake.
Wapo wanaoimezea mate Tanzania na kutamani utulivu na umoja ilionao. Yumkini, wapo wanaoiombea mabaya Tanzania ili eti iingie katika mgawanyiko na pengine katika vita. Katu Watanzania tusikubali kuruhusu dua hizo zitupate. Sote tuwe imara na makini wakati wote katika kujilinda na kulinda taifa letu ili tusigawanywe.
Tukumbuke kuwa, wakoloni wa Kiingereza walitumia mkakati wa ‘divide and rule’ yaani ‘wagawe, uwatawale.’ Mbinu hii ina nguvu kubwa kudhoofisha na kupotosha wananchi wasiwe na umoja wala upendo wao kwa wao. Sote tunaelewa kuwa umoja ni nguvu na upendo ni ukamilifu wa yote. Umoja na upendo ni silaha ziletazo uimara wa taifa na ustawi wa jamii.
Nasema hivyo kwani kwa mtazamo wangu, taifa letu limekumbwa na roho ya chuki na kunyosheana vidole sisi kwa sisi. Kubwa linalosababisha kuchukiana na kunyosheana vidole, ni kinachoitwa ‘kudai haki’. Hapa, tukumbushane maana ya neno ‘haki.’
Hii ni nomino ya kifalsafa katika matawi yake ya maadili (adala), sheria, dini, stahiki na busara. Kwa mujibu wa Shule za Mfalme Justinian (Institutes of Justinian), tangu Karne ya Sita, ‘Haki’ ihutafsiriwa kuwa ni utashi endelevu wa kumtendea mtu anavyostahili.
Kwamba, watu wanapaswa kutendewa bila upendeleo, kwa njia inayofaa kwa mujibu wa sheria na wakati mwingine mbele ya vyombo vya kutoa haki na wasuluhishi. Kwa mtazamo wangu, tunapozungumzia haki za binadamu, tunazungumzia pia kulinda utu wa binadamu kwa uadilifu, ndiyo maana katika utu wa mtu, haki ya kwanza kabisa ni haki ya uhai/kuishi, ya pili ni uhuru na ya tatu ni heshima.
Katika haki zote za binadamu, haki ya msingi ni haki ya kuishi au ya uhai. Uhai wa mtu yeyote duniani unalindwa na heshima na usalama. Bila heshima na usalama, uhai wa mtu unakuwa hatarini. Vilevile uhai au maisha ya mtu bila heshima hayana maana. Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kuheshimu wengine hapo ndipo inaelezwa kuwa haki ni neno la adala (kimaadili).
Katika haki hizi zilizojikita kusimamia watu ni muhimu kila tunapodai au kutoa haki kuzingatia maadili. Tukienda kinyume na hayo, moja kwa moja Sheria Mvuto (Law of Attraction) itatupa stahiki yetu. Maana yake ni kuwa, unapodai au kutoa haki bila kujali maadili yaani nidhamu, utajikuta umezua taharuki na kusababisha Sheria Mvuto kufanya kazi yake.
Mara nyingi katika mazingira hayo, huwa inavuruga na kuwaachia watu maumivu na uchungu mkubwa na wengine hupoteza maisha. Sheria Mvuto katika mazingira ya kudai haki, mara nyingi hutokea pale ambapo wahusika wanatumia mabavu na lugha chafu kudai au kutoa haki za msingi.
Turejee mfano huu: Mtu mmoja alimwazima jirani yake jembe kwa makubaliano kuwa baada ya kumaliza kazi
lingerejeshwa kesho yake asubuhi. Kesho yake mchana jembe halikuwa limerejeshwa.
Mwenye jembe (Mdai) aliondoka na kumfuata aliyemwazimisha jembe na alipofika bila kujua wala kuuliza sababu za kuchelewa kurejesha jembe lake; akamtukana na kumkashifu kwa kelele nyingi jirani yake (Mdaiwa) huku akimsonga kutaka kumpiga mbele ya watu waliokuwepo.
Yule mdaiwa naye alipoona kuwa amedhalilishwa na utu wake kutwezwa mbele ya kadamnasi, akakasirika na akahisi yuko hatarini kupigwa. Akamfungulia mbwa wake. Mbwa huyo akamshambulia na kumyejeruhi mwenye jembe.
Baada ya kuumizwa na mbwa, ndugu zake walikuja na kulalamika, wakimchukia mdaiwa kuwa ni mtu wa dhuruma na asiye na utu. Hawakutaka kujua sababu ya yule mdaiwa kumfungulia mbwa wake. Wao alimwangalia aliyeumizwa na mbwa na kumhurumia bila kujua sababu iliyomfanya mdaiwa kumfungulia mbwa wake.
Wataalamu wa Haki na Sheria wanasisitiza umuhimu wa kusikiliza pande zote na kuhakikisha unapata taarifa za kutosha pande zote kabla ya kutoa lawama au hukumu. Hapa, tunajifunza kudadisi kilichosababisha Sheria Mvuto kuingilia Sheria Msingi.
Kimsingi, suala la haki ya heshima na kulinda utu wa mtu lilikiukwa wakati mwenye jembe akidai haki ya kupewa
mali yake ndio maana sheria mvuto ikaingilia kati kulinda kwa nguvu kubwa haki ya heshima ambayo ni haki inayosimamia haki zote za binadamu.
Katika kudai haki unaweza ukachelewesha au kupoteza haki zako kutokana na njia unayoitumia kudai haki husika. Hivyo, Watanzania tusisahau kuheshimiana katika kudai au kutoa haki.
Tusipozingatia maadili kwa kuwa na nidhamu katika kufuata sheria, kanuni na taratibu tutapata haki tusizozitarajia wala kustahili kupata na hapo, tutaanza kulaumiana hatimaye kujikuta tunawapa adui zetu nafasi za kutuingilia, kuzua taharuki na pengine hata kutusambaratisha.
Tujitahidi kuwa wastahimilivu, wenye nidhamu na tunaoheshimiana wakati wote. Daima tukumbuke kuwa, watu ni rasilimali yenye thamani kubwa kuliko rasilimali yoyote ulimwenguni. Thamani ya watu hutokana na heshima. Uhai bila heshima hauna maana, ndio maana wengine hujiua kwa sababu ya aibu/kupoteza heshima kwani heshima ya mtu ndio utu.
Hata hivyo, kujiua kwa sababu yoyote si jambo jema kiroho, kijamii na hata kisheria. Hiyo ndio hutofautisha mtu na mnyama au vitu vingine. Ni muhimu kulinda heshima ya mtu kwa wivu mkubwa kuliko rasilimali yoyote. Kwa msingi huo nasema Kwa Mtazamo Wangu, kuhusu Suala la haki, kila mmoja wetu ajue analo eneo lake la kutoa na kupewa haki.
Katika eneo lake, kila mmoja azingatie nidhamu na usalama wakati wote wa kudai au kutoa haki. Nidhamu na usalama ndiyo nguzo za amani na utulivu wa nchi.
Kudumisha upendo
Watanzania hasa wazazi, wazee na viongozi wote bila kusahau viongozi wa dini, tuhakikishe tunasimamia vizuri vyanzo vya kudumisha na kuhimiza upendo. Mafundisho ya upendo yanapatikana katika familia na katika mafundisho ya kiimani. Aidha, kila kiongozi wa familia ahakikishe anasimamia na kueneza kwa vitendo suala la upendo wa dhati.
Upendo ukiimarika katika familia, tutapunguza kunyosheana vidole na kuchukiana bila sababu na hivyo tutathaminiana na kuishi kwa umoja, upendo, ushirikiano na kubwa zaidi, kuheshimiana. Katika hali ya kawaida, taasisi haziruhusu mtu amchukie mwingine, au akiuke taratibu na kanuni za kiutu. Kuchukiana au kufanya matendo mabaya ni matokeo ya hulka za mtu binafsi na si taasisi.
Kwa mtazamo wangu ili kulinda taifa letu dhidi ya watu wabaya, tusinyoshee vidole wala kuchafua taasisi zetu kwa mabaya yatendwayo na wachache. Linapotokea tatizo, tufuatilie mienendo na mazingira ya mtu au watu husika, watuhumiwa wanapopatikana wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria kwa ajili ya kutoa hukumu stahiki.
Kuishi na wenzetu
Tujitahidi kuishi katika Kanuni ya Dhahabu (Golden Rule) ya kutenda kama tunavyotaka kutendewa. Wakati wote palipo na mgogoro, tujitahidi kuwa wapatanishi kuliko kuwa wachonganishi au wagombanishi maana, “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu”.
Sote tusisitize mafunzo ya upendo na heshima ili tuliponye Taifa dhidi ya taharuki zinazotokana na mitandao ya kijamii. Inapotokea migogoro kwa walio chini yetu tujitafakari katika mafunzo yetu ya upendo; tukae chini tupange mbinu madhubuti za kuimarisha upendo. Hapo tutakuwa tumeangamiza roho za mabaya ikiwemo chuki, migogoro na kunyosheana vidole.
Ulinzi wa maadili
Kama ilivyoanzishwa Sheria maalum ya Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kulinda uchumi wa taifa, pia iundwe sheria madhubuti ya Ulinzi wa Heshima ya Utu wa Mtu ili kusaidia watu kusimamia haki hii muhimu kwani uhai bila heshima hauna maana, kwa kuwa utu wa mtu umekufa.
Sheria hii itasaidia kulinda maadili na kukabili changamoto za kimaadili zinazotokana na malezi mabaya ya watoto na matumizi hasi ya mitandao ya kijamii.
Mwandishi ni Daktari wa Maendeleo ya Binadamu na Mbobevu wa Afya Bora ya Akili. Wasiliana naye kwa
baruapepe: mayrosekm@gmail.com