Hiki ndicho wanachojivunia wanawake wanaotumia uzazi wa mpango

WAKATI leo mashirika ya serikali, sekta ya binafsi, vyombo vya habari, na watu binafsi wanaadhimisha Siku ya Uzazi wa Mpango, baadhi ya wanawake wameelezea namna njia hiyo ya uzazi wa mpango ilivyowasaidia kupanga maisha yao na familia zao.

Wanawake hao waliozungumza na  HabariLeo hivi karibuni walielezea ndoto zao za kujenga familia wanayoweza kumudu kuitunza na yenye maisha bora katika maeneo muhimu ya elimu, chakula, afya na malazi.

Mkazi wa Kawawa Halmashauri ya Dodoma Veronica Tumaini (26) alisema pamoja na kwamba anatumia uzazi wa mpango kwa kificho dhidi ya mumewe, umemsaidia kupangilia uzazi wake tofauti na alivyokuwa akitaka mumewe.

Advertisement

Veronica mwenye watoto watatu, mmoja ana umri wa miaka tisa, mwingine minne na mdogo miezi tisa, alisema alianza matumizi ya uzazi wa mpango baada ya kushauriwa na mama yake mzazi atumie njia ya kuweka kijiti, lakini mumewe hakutaka uzazi wa mpango. Alimtaka azae mtoto mwingine kila mtoto wao atakapofikicha umri wa mwaka mmoja na nusu.

Alisema alipoenda kliniki baada ya kupata mtoto wake wa kwanza, alipata mafunzo kuhusu njia ya mpango na kuamua kuweka kijiti lakini mumewe alipoona anachelewa kupata mimba alimkagua mwilini na kumkuta na kijiti hicho na kumlazimisha akitoe.

Alipotoa ndipo akapata mtoto mwingine wa pili alipoenda tena kliniki akaweka kijiti na mumewe aliposhtukia akalazimisha atoe ndipo akapata tena mtoto wa tatu mwenye umri wa miezi tisa sasa.

Alisema mtoto wake huyo alipofikikisha miezi minne aliweka tena kijiti na kuahidi kuwa mumewe akimshtukia tena hatokubali kutoa kijiti hicho na yuko tayari kupelekana hadi kwenye vyombo vya sheria.

Esther Logan (25) naye kutoka kijiji cha Kawawa ana watoto watatu wa kwanza mmoja akiwa amemzaa akiwa na umri wa miaka 19 baada ya kuolewa, alisema alianza kutumia uzazi wa mpango baada ya kumshirikisha mumewe na kukubaliana kutokana na hali yake ya maambukizi ya Ukimwi.

Alisema alitumia njia ya kuweka kipandikizi lakini alilazimika kubadilisha baada ya kukosa nguvu kwa sababu ya dawa za HIV anazotumia na kutumia njia ya sindano mpaka sasa.

Ana watoto watatu mmoja ana miaka sita, wa pili miwili na wa mwisho miezi saba.

Alisema mumewe hana HIV yuko vizuri na alianza kujihusisha kimapenzi tangu akiwa na umri wa miaka 17 kutokana na ushawishi wa marafiki.

Esther ni mkulima wa zabibu na anawashauri wasichana wenzake kutumia uzazi wa mpango ili kuwa na familia wanayoweza kuihudumia vizuri. Lakini pia anaomba elimu juu ya maambukizi ya Ukimwi iendelee kutolewa ili kuokoa watu wengi kupata maambukizi.

Neema Stanley (24) kutoka Kijiji cha Mapinduzi ana watoto wawili, alisema alianza kutumia njia ya mpango baada ya kwenda kliniki ambako alipatiwa elimu juu ya afya ya uzazi.

Baada ya kuelimishwa aliamua kutumia njia ya mpango ya sindano. Ni mkulima wa karanga na alizeti.

Kwa upande wake Muuguzi wa Afya ya jamii katika zahanati ya Mpunguzi Dodoma Vaselina Mrema, aliishukuru serikali kwa kuwa na mpango wa elimu ya uzazi wa mpango inayosaidia katika zahanati hiyo kwa siku kupokea wanawake 50 hadi 60 wanaotaka husuma hiyo.

Hata hivyo, alishauri kuwepo na hamasa kubwa kwa wanaume kuhusu suala hilo ili wawe na mwitikio chanya katika suala hilo la uzazi wa mpango.

Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma Dk Mfaume Mursal alisema wamekuwa wakitoa elimu ya mpango huo katika maeneo mbalimbali katika jiji hilo kupitia kliniki za wazazi kwenye vituo vya afya ili kufikia familia nyingi zaidi na mwitikio ni mzuri.

Alisema uzazi wa mpango ni njia nzuri ya kupanga familia lakini pia inamsaidia mwanamke kupanga uzazi wake kwa kutunza afya yake.

Takwimu zinaonesha asilimia 32 tu ya wanawake nchini walio katika umri wa uzazi wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango huku asilimia 22 wakiwa na mahitaji ambayo hayajafikiwa.

Vifo vya uzazi nchini Tanzania viliongezeka hadi vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2010.

Kwa kuzingatia kanuni zilizopo zinazowaweka wasichana kwenye ngono za utotoni na ndoa za utotoni, asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 19 na 15 ni wajawazito au wameanza kuzaa.