Hili la wageni 12 kucheza katika mechi moja linahitaji mjadala

MAPEMA wiki hii Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepitisha kanuni ya kutumia wachezaji 12 wa kigeni katika mchezo mmoja kwa timu za Ligi Kuu.

Ikumbukwe kuanzia msimu uliopita idadi ya wachezaji wa kigeni ilikuwa ni 12 na wanaoruhusiwa kucheza katika mchezo mmoja ni wanane. Kanuni hiyo ni kama inakwenda kutengeneza makundi ya timu kwenye ligi kwa maana kwamba zipo timu chache zenye uwezo wa kifedha ndizo zitakazopambana kufukuzia ubingwa kila siku.

Kanuni hiyo imezibagua timu za daraja la chini ambazo bajeti yake kwa msimu haifiki hata Sh milioni 400. Kuruhusu kanuni hii itumike ina maana unatengeneza timu ya taifa ‘Taifa Stars’ dhaifu.

Lakini ukiacha hilo kuruhusu wachezaji 12 wa kigeni kutumika kwenye mchezo mmoja ni kupoteza vipaji vya wazawa, ambavyo mara nyingi huwa havithaminiwi na wanakuwepo kama ziada katika klabu husika. Katika hili TFF ilipaswa kulifanyia upembuzi kwa kina kabla ya kulipitisha na kuanza kufanya kazi.

Inawezekana lengo lao likawa jema kwa maana ya kuongeza hamasa, lakini hilo haliwezekani sababu wenyewe tunajijua asili yetu. Imepenya haisapoti ujinga lakini katika hili wahusika ambao ni Bodi ya Ligi na TFF, walipaswa kuliangalia kwa makini kwa masilahi ya timu ya taifa.

Mataifa yaliyopiga hatua na ligi zao maarufu duniani bado hazitumii mfumo huo wa kutumia wachezaji wageni wote inakuwaje Tanzania nchi ambayo hata kufuzu Afcon inakuwa mtihani. Yawezekana wahusika TFF na Bodi ya Ligi wamewekeza nguvu kwenye kuitangaza ligi ili kujulikana zaidi, lakini hiyo haitoshi kuwa kigezo cha kujaza wageni kwenye mchezo mmoja.

Kwa hiki walichokiamua TFF tutegemee kuiona Simba ikimtumia Aishi Manula peke yake siku inacheza na Al Ahly. Au tusitarajie kumuona Bakari Mwamnyeto, Dickson Job au Denis Nkane siku Yanga wanacheza na Al Hilal. Ni kweli lengo la kila kiongozi wa TFF ni kutengeneza sifa nzuri ili aweze kupongezwa na wakubwa Caf na Fifa lakini katika hili sidhani kama wapo sahihi.

Hiyo ilitokana na uzoefu wa mechi za kimataifa waliokuwa nao wachezaji hao kutokana na timu zao kushiriki mara kwa mara mashindano ya kimataifa. Pamoja na yote wachezaji wazawa nao wanapaswa kuichukulia hiyo kama changamoto na wanapaswa kujipanga ili kugombea namba na wageni kwenye timu zao.

Habari Zifananazo

Back to top button