HONGERA Kamati maalumu inayohusika na kuwasimamia waamuzi kutokana na mwanzo mzuri ambao wameanza nao kwenye msimu huu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mpaka wakati huu ambapo ligi imesimama kupisha maandalizi ya Taifa Stars kufuzu fainali za Chan, hakuna klabu yoyote ambayo imelalamika kuhusu mwamuzi.
Tofauti na misimu iliyopita ambapo mpaka kufika sasa raundi ya pili kulikuwa na malalamiko ya kutosha kuhusu maamuzi mabaya ya waamuzi.
Ndio maana tunaipongeza kamati husika chini ya Mwenyekiti wake, Soud Abdi kwa kufanya kazi kubwa ya kupunguza kasoro hiyo, ambayo kwa kiasi fulani ilipoteza ladha ya soka nchini.
Achana na semina na mafunzo ambayo huwa ni kawaida kuyapata kila msimu mpya unapotaka kuanza, lakini kuna kitu cha ziada ambacho yawezekana Soud amekipandikiza kwa waamuzi wetu msimu huu.
Huko nyuma matukio tata na ya dhuluma yalikuwa ya waziwazi na timu nyingi hasa ndogo ziliumizwa na kitu hicho mbaya zaidi hakukuwa na utetezi wa msingi.
Ingawa ni mapema sana kuwasifia lakini kwa mwanzo walioanza nao msimu huu wanastahili pongezi kutokana na kile walichokionesha kwenye mechi raundi mbili za mechi za ligi kuu.
Lakini wakati tunawapongeza waamuzi ni wakati huu ndio tunatumia kuwaasa kuendelea na mwenendo mzuri ambao wameanza nao msimu huu.
Wasibadilike na kusababisha lawama ambazo kiasili zinaharibu ubora wa ligi yetu ambayo kwa sasa ni maarufu kutokana na ushindani uliopo lakini pia mishahara mikubwa ambayo wachezaji wanalipwa.
Itapendeza kuona ligi inakuwa maarufu lakini pia lawama kutoka kwa timu kwenda kwa waamuzi zinapungua kama si kumalizika kabisa.
Sababu kufanya kwao vibaya ndio kunasababisha athari nyingi kwao ikiwemo kutojumuishwa kuchezesha mashindano makubwa ya Afrika na hata duniani.
Kwa upande wa TFF kuna haja ya kusaidiana na Kamati ya Waamuzi kurekebisha hili la waamuzi.
Inadaiwa wana malimbikizo ya madeni kwa misimu kadhaa hebu walipeni madeni yao ili akili zao zihamie mchezoni.
Waamuzi wanatakiwa kuithamini kazi yao sababu ndio waliyoichagua ingawa ni kweli kwamba kutolipwa kwa wakati kunapunguza utendaji na ufanisi lakini pia kuharibu kazi kwa kucheweleshewa malipo kunapoteza sifa na kukushusha daraja.
Wapo baadhi ya waamuzi wamekuwa wakiogopwa na viongozi wa timu fulani kutokana na maamuzi ya utata pindi wanapozichezesha timu zao kiasi cha kuiomba Bodi ya Ligi kutowapanga wachezeshe mechi zao.
Sasa kwa mwamuzi anayejitambua na mwenye malengo ya kufika mbali hiyo si ishara njema na inakuharibia sifa na kuwatukanisha wale ambao wamekuamini na kukupa beji ya Fifa ambayo kwa Tanzania ni waamuzi wachache ndio wanayo.
Ifike wakati waamuzi pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kucheleweshewa posho zao lakini watumie taaluma yao kutenda haki wanapokuwa uwanjani.