KIGOMA: Kutekelezwa kwa mpango wa kliniki tembezi maarufu kama Mkoba ya huduma za kinga, tiba na matunzo (CTC) kupitia shirika la THPS, imewezesha kufikiwa kwa idadi kubwa ya wapokea huduma wanaoishi na maambukizi ya VVU maeneo ya pembezoni kwa kuwawezesha kupata dawa na kuzitumia kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa Afya Hatua Wilaya ya Uvinza Dk Gabriel Max, wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani humo iliyolenga kuangalia utekelezaji wa mradi wa afya hatua unaotekelezwa na shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa Ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).
Dk Max amesema kuwa huduma ya mkoba imesaidia wapokea huduma kufika kwenye maeneo yaliyotengwa kwa wakati kupata huduma, kupata dawa kwa wakati na sasa wanafuata ratiba kikamilifu kwa siku za kupata dawa, hivyo kufubaza VVU na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo baada ya afya zao kuimarika.
Akizungumza katika ziara hiyo muuguzi kutoka kituo cha Afya Uvinza, Dk Said Hamis Said amesema kituo cha afya Uvinza kinahudumia wateja 780, ambao wana maambukizi ya VVU na sehemu ambayo wanapokea wateja wengi ni kutoka kwenye vituo vya Huduma Mkoba ikiwemo Tandala, ambako hakuna kituo chochote cha kutoa huduma za afya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tandala kwenye Kijiji cha Chakuru wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Ngasa Kamishe amesema kuwa kuwepo kwa huduma ya Mkoba kwenye kitongoji hicho, imesaidia walengwa kupata huduma kwa urahisi, kwa wakati, lakini pia kupunguza gharama kutembea umbali wa kilometa 50 kufuata huduma kituo cha afya Uvinza.