Huduma ya mizigo SGR yaanza rasmi Dar -Dodoma

DODOMA: SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema kukamilika kwa asilimia 98.6 ya ujenzi wa kipande cha pili cha Reli ya kisasa ya mizigo ya (SGR) kumewezesha kuanza rasmi kwa huduma ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi stesheni ya Bahi mkoani Dodoma kwa masaa matano.

Pia huduma hiyo italeta mapinduzi na ufanisi katika sekta ya usafirishaji, kupunguza gharama za biashara na kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi pamoja kuwasaidia wafanyabiashara kupata mizigo yao kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya TRC, mhandisi wa mradi huo, Christina Samuel alisema huduma ya usafirishaji wa mizigo ilianza Juni 26, mwaka huu baada ya kukamilika kwa kiwango hicho cha ujenzi.

Aliongoza kuwa stesheni hiyo ipo katika kipande hicho cha pili cha mradi wa SGR unaoanzia mkoa ha Morogoro hadi Makutupora Dodoma.

Alisema kwa sasa mizigo inasafirishwa kwa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Bahi, na kuhamishiwa kwenye reli ya zamani (MGR) kwa ajili ya kuendelea na safari kuelekea Kigoma, Isaka Shinyanga, Mwanza na maeneo mengine yanayohudumiwa na mtandao huo.

Aliongeza kuwa behewa moja lina uwezo wa kubeba tani 56 za mizigo sawa na makontena mawili yenye tani 28 kila moja, huku kwa sasa treni moja ikisafirisha makontena 20 kwa safari.

Aidha alisema stesheni ya Bahi ina uwezo wa kuhifadhi makontena 1,500 kwa wakati mmoja uwezo unaofanana na wa stesheni ya Ihumwa, hali inayowezesha kuhudumia idadi kubwa ya wateja.

Alieleza kuwa matumizi ya reli ya mizigo ya SGR yanapunguza gharama za uendeshaji kwa kuwa treni zinatumia nishati ya umeme badala ya mafuta huku pia yakisaidia kupunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara unaosababishwa na malori yenye mizigo mizito.

Kuhusu usalama wa mizigo Christina alisema stesheni zote zimewekewa mfumo wa kamera za ulinzi (CCTV), zimezungushiwa uzio na zinalindwa na walinzi wa kutosha ili kuhakikisha mali za wateja zinakuwa salama wakati wote.

“Tunawahakikishia wadau wote kuwa mizigo yao ipo salama na miundombinu ya usalama imeimarishwa na tunaendelea kutoa huduma kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wateja,” alisema Christina.

Alitoa mwito kwa wafanyabiashara, waagizaji na wasafirishaji wa mizigo kutumia huduma ya reli ya SGR, akisisitiza kuwa ni njia salama, ya haraka, yenye uhakika wa muda na gharama nafuu huku ikichangia kuongeza ufanisi wa biashara na kukuza uchumi wa taifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button