MOJA kati ya haki ya msingi za kila binadamu ni kufurahia viwango vya juu vya afya viwezekanavyo. Serikali zina majukumu ya kitaifa na kimataifa kutoa huduma bora za afya zinazofikika kwa gharama nafuu na zinazopatikana kwa watu wote bila ubaguzi.
Hata hivyo, uhalisi huu katika nchi zinazoendelea kama vile katika Afrika Mashariki ni matakwa ambayo bado hayajatimia. Kanuni kuu ni kwamba haki ya afya inategemea upatikanaji wa rasilimali za serikali. Ingawa serikali katika ukanda huu zimeweza kuzongwa na ukosefu wa rasilimali na kushindwa kutoa huduma jumuishi za afya kwa watu wote, huduma za afya kwa masikini na wale walioathirika si hiari bali wajibu.
Aidha, serikali zinalazimika kuendelea kupanua utoaji wa huduma ya afya kila mwaka na ni mzigo uko begani mwa serikali kuonesha kwamba inafanya hivyo na kwa upeo wa rasilimali zilizopo.
Leo ni siku ya kimataifa ya huduma za afya kwa wote ambapo Umoja wa Mataifa umeweka mkazo suala la huduma ya afya kwa wote. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Ghebreyesus anasema suala la huduma ya afya kwa wote ni lengo kuu la shirika hilo akisema hatua muhimu ya kufanikisha ni kuhakikisha kila mtu anapata huduma anayohitaji, pindi anapohitaji palepale kwenye jamii yake.
Anasema, ingawa kuna maendeleo yamefikiwa katika baadhi ya nchi mbalimbali duniani kuona kila mtu anapata huduma ya afya, bado mamilioni ya watu wanalazimika kuchagua kati ya huduma ya afya na mlo, mavazi au hata makazi.
“Tupo hapa kuweka kauli thabiti kuwa afya ni haki na si upendeleo. Tupo hapa kusema kuwa watu wote wana haki ya kupata huduma ya afya wanayohitaji, pindi wanapohitaji bila mkwamo wowote wa kifedha,” anasema mkurugenzi mkuu huyo wa WHO wakati wa tukio maalumu lililofanyika mjini Geneva, Uswisi. Anaongeza kuwa, WHO ndiyo mwamba wa huduma ya afya ya msingi kwa wote na kwamba, “Huduma ya afya ya msingi kwa wote inahusisha mahitaji yote makubwa ya afya ya binadamu.
Inasaidia pia kuepusha watu kwenda hospitali na kusalia kwenye jamii zao.” Kwa mantiki hiyo, katika siku hii ya kimataifa ya huduma za afya kwa wote mwaka huu wa 2022, wanazidi kutoa wito kwa mataifa kuwekeza katika huduma za msingi za afya.
Mkurugenzi mkuu huyu wa WHO anakumbusha kuwa maadhimisho haya, yamaanishe kwa vitendo na serikali zihakikishe watu wote na jamii wanapokea huduma za matibabu wanazohitaji bila kutatizika kifedha.
Huduma ya afya kwa wote inawezesha kila mmoja kupata huduma zinazohusiana na sababu kuu za chanzo cha maradhi na vifo, na kuhakikisha kuwa ubora wa huduma hizo unafaa kuimarisha afya ya watu wanaozipokea. Kufaulisha mpango wa huduma ya afya kwa wote ni mojawapo ya malengo yaliyowekwa na mataifa mbalimbali duniani yalipokubali Malengo ya Ustawi Endelevu mnamo 2015.
Nchi ambazo zimepiga hatua katika huduma ya afya kwa wote zitapiga hatua pia katika mambo mengine yanayohusiana na afya na maendeleo.
Afya njema huwezesha watoto kusoma na watu wazima kupata mapato. Katika nchi ambapo huduma za afya kwa kawaida zimekuwa zikipatikana na kwa gharama nafuu, serikali zinaendelea kukabiliana na changamoto za kushughulikia mahitaji ya afya yanayozidi kuongezeka ya wananchi na gharama zinazoongezeka za huduma za afya. Kuelekea kufaulisha huduma ya afya kwa wote kunahitaji kuimarisha mifumo ya afya katika nchi zote.
Miongozo thabiti ya ufadhili ni muhimu. Watu wanapohitajika kulipa gharama nyingi za huduma za afya kutoka mifukoni mwao, masikini mara nyingi hushindwa kupata huduma wanazohitaji na hata wanaojiweza huenda wakapata ugumu wa kifedha iwapo magonjwa yatazidi au kuchukua muda mrefu kupona.
Kuimarisha kuwepo kwa huduma za afya na matokeo ya afya hutegemea uwepo, ufikiaji na uwezo wa wahudumu wa afya kutoa huduma bora za pamoja kwa watu.
Uwekezaji katika huduma bora za afya za kimsingi utakuwa njia kuu ya kufaulu huduma ya afya kwa wote duniani kote kwani ni njia yenye gharama nafuu.
Uongozi bora, mifumo thabiti ya uagizaji na usambazaji dawa na teknolojia za afya pamoja na mifumo inayofanya kazi ya habari kuhusu afya ni masuala mengine muhimu.
Kutimiza mahitaji ya wahudumu wa afya ya Malengo ya Ustawi Endelevu na huduma za afya kwa wote, wahudumu wa afya wa ziada wanaozidi milioni 18 wanahitajika kufikia mwaka 2030. Ongezeko la hitaji la wahudumu wa afya linakadiriwa kuongeza takribani nafasi milioni 40 za kazi katika sekta ya afya kwenye uchumi wa dunia kufikia mwaka 2030.
Uwekezaji unahitajika kutoka kwa sekta za umma na binafsi katika elimu ya wahudumu wa afya, pamoja na kuunda na kujaza nafasi zinazofadhiliwa katika sekta ya afya na uchumi wake.
Huduma za afya, ambazo ni pamoja na matibabu ya dawa za kienyeji na za kisasa, zikiratibiwa kwa kuegemea mahitaji kamili na matarajio ya watu na jamii zitasaidia kuhamasisha na kuwafanya kujihusisha zaidi katika afya yao na mfumo wa afya. Mambo muhimu kuhusu huduma ya afya kwa wote Takribani nusu ya wakazi wa dunia bado hawapati huduma za msingi za afya.
Watu milioni 100 bado wapo kwenye ufukara kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia huduma za afya. Zaidi ya watu milioni 800, sawa na asilimia 12 ya wakazi wote wa dunia, wanatumia asilimia 10 ya kipato cha kaya kugharimia huduma za afya.
Mataifa yote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa wamekubaliana kufikia lengo la huduma ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
0685 666964 au bjhiluka@
yahoo.com.