NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Sauda Msemo amesema Serikali kupitia benki hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi kwa gharama nafuu.
Sauda amebainisha hayo leo kwenye hafla ya kusheherekea miaka 25 ya Benki ya NMB, iliyoambatana na kutoa gawio kwa Serikali.
“Benki kuu ina dhamana ya kusimamia sera za uchumi hapa nchini tunapenda kuhakikisha kuwa tunaendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa letu,” amesema Sauda.
Awali akizungumza katika tukio hilo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Tanzania ,Ruth Zaipuna amesema benki hiyo ina matawi 227, mashine za ATM 781, mawakala 23,679 na akaunti za wateja milioni 6.3 ukilinganisha na akaunti laki 6 zilizokuwepo mwaka 1997.
Amesema mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi yaliyopo nchini yanayopelekea ukuaji wa uchumi na makampuni ikiwemo Benki ya NMB.