Hukumu rufaa kesi ya kiraia mbioni kutolewa

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Rufaa ya Tanzania kwa mara ya kwanza imesikiliza kesi ya haki za binadamu ya kupinga vikwazo katika mashauri ya umma mahakamani ambapo hukumu itatolewa mara baada ya maombi ya waleta mashtaka na wajibu mashtaka kupitiwa na majaji.

Kesi hiyo ya Rufaa ya Kiraia Na.134 ya mwaka 2022, inayomhusisha mtetezi wa haki za binadamu, wakili Onesmo Olengurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inasikilizwa na majaji watatu ambao ni Jaji Levira, Jaji Rumanyika na Jaji Ngwembe.

Wakili Mkuu wa Serikali, Hangi Chang’a mara baada ya kusikilizwa kesi hiyo amesema mlalamikaji alifungua shauri kwa sababu hakuridhika na hukumu ya mahakama kuu na amekata rufaa na mahakama imesikiliza sababu sita ikiwemo haja ya kuwepo kiapo cha kuathirika kwa mlalamikaji na zingine.

“Tumewasilisha mawasilisho yetu na mahakama imetupa muda wa kutosha hivyo mahakam itatoa tarehe ya kutangaza maamuzi yake tumeiachia.

Kwa upande wa mleta mashtaka uliongozwa na jopo la mawakili wanne ambao ni Prof Issa Shivj, wakili Mpale Mpoki, Dk Rugemeleza Nshala na Wakili John Seka.

Akizungumza wakili Dk Nshala amesemasheria iliyobadilishwa inataka mlalamikaji aoneshe ni jinsi gani anayelalamika ameguswa vipi binafsi na ukikwaji huo na mahakama kuu ilipitia ikasema hakuna kosa ya Sheria na Olengurumwa akakata rufaa na imesikilizwa leo.

“Jopo letu limeongozwa na Prof Issa Shivji mahakama imetupatia muda wa kutosha kutoa ufafanuzi na kujibu maswali mbalimbali hukumu haijatoa mahakama imesema inahitaji muda wa kwenda kuchambua hoja zetu na kuziangalia na itatoa hukumu yake siku na tarehe watakayoitaja.

Aidha Wakili Olengurumwa ameeleza sababu ya kufungua shauri la kupinga uhalali wa kikatiba wa marekebisho ya kifungu cha saba cha Sheria ya utekelezaji wa haki za msingi na wajibu (BRADEA) ambayo yalifanyika kupitia marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba tatu ya mwaka 2020.

Amebainisha kuwa mahakama imetoa nafasi nzuri ya kusikiliza kesi ambapo ameelzea kuwa
Mahakama ni chombo cha kikatiba kwa yoyote yule ambaye anaona haki imevunjwa anapaswa kwenda.

“Na sisi kama watetezi wa haki za binadamu tuna njia mbili za kutetea haki za watu kwanza ni mahakama na kushawishi serikali kwahiyo katiba imetoa nafasi kwa sisi kupitia taasisi,mtu moja moja au mtetezi endapo ataona haki imevunjwa atakwenda mahakamani lakini bahati mbaya mwaka 2020 Sheria ikatugwa na ikatupoka haki hiyo kumtetea mtu ambaye hana uwezo wa kujitetea.

Msingi wa kesi hiyo ni kwamba, Mnamo tarehe 19 Juni 2021, Serikali ya Tanzania ilichapisha katika gazeti la serikali Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya mwaka 2020, iliyofanya mabadiliko makubwa katika Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu kwa kuongeza vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5).

Kifungu cha 4(2) kinahitaji kila mtu anayepeleka shauri Mahakama Kuu kuhusu ukiukwaji wa haki za kikatiba kuambatanisha kiapo kinachoeleza jinsi alivyoathirika binafsi na kifungu cha 4(3) kinabana zaidi mashauri ya maslahi ya umma kwa kutaka mlalamikaji kuonyesha maslahi binafsi kwa mujibu wa Ibara ya 30(3) ya Katiba.

Aidha, Kifungu cha 4(4) kinahitaji kwamba pale mtu anapotafuta haki dhidi ya viongozi wa juu serikalini, wakiwemo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu, kesi ipelekwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu badala ya viongozi hao moja kwa moja.

Vilevile, Kifungu cha 4(5) kinataka mlalamikaji kutumia njia zote nyingine za kisheria zilizopo kabla ya kufungua kesi chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu.

Baada ya kupelekwa mahakamani kwa shauri hilo, Mahakama Kuu ya Tanzania Mnamo tarehe 15 Februari 2022 ilitoa uamuzi wake na kusema kuwa vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5) vya Sheria hiyo havipingani na Katiba wala mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button