IAA yawekeza bilioni mbili kwenye teknolojia

CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA) kimetenga Shilingi bilioni 2 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya kiteknolojia na kidijitali, hatua inayolenga kubadili mfumo wa utoaji elimu na kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu miradi ya maendeleo na fursa za vijana kwa mwaka 2025/2026, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema uwekezaji huo unahusisha uanzishwaji wa Madarasa Mahiri yanayotumia Akili Unde (AI Smart Classrooms) katika kampasi za chuo hicho.
Amesema madarasa hayo yana ubao shirikishi wa kidijitali, mifumo ya kurekodi mihadhara kwa usaidizi wa AI, uchambuzi wa papo kwa papo wa ushiriki wa wanafunzi na mifumo ya kisasa ya kufuatilia mahudhurio, hali inayomwezesha mhadhiri kubinafsisha ufundishaji kwa kutumia takwimu za ujifunzaji huku wanafunzi wakipata uzoefu wa elimu shirikishi na jumuishi, ikiwemo kwa wanafunzi wa masafa.
Aidha, chuo kinaanzisha Kituo cha Kisasa cha Data kitakacholinda taarifa za kitaasisi, kusaidia majukwaa ya ujifunzaji yanayotumia ‘cloud’, kuhifadhi data za utafiti na kuimarisha usalama wa mtandao, hatua itakayopunguza utegemezi wa huduma za upangishaji wa nje na kuimarisha uhuru wa kidijitali. SOMA: Tanzania yaendelea kupiga hatua teknolojia kilimo
Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa IAA pia inatekeleza mfumo wa Elimu Mseto (Blended Learning) unaounganisha masomo ya ana kwa ana na mtandaoni kupitia LMS na zana za tathmini za kidijitali, akibainisha kuwa mageuzi hayo yataongeza ujumuishwaji wa elimu, kuwafikia wanafunzi wa maeneo ya mbali na kuzalisha wahitimu wenye umahiri wa kidijitali na ushindani wa kimataifa.



