INEC: Waandishi kiungo muhimu elimu ya mpiga kura

DAR ES SALAAM; MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, amesema waandishi wamekuwa kiungo kikubwa kupitia taarifa za habari, vipindi na makala katika kutoa elimu ya mpiga kura.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kuwafikia walengwa kote nchini ili waweze kupata taarifa ya nini wanapaswa kufanya kwa mustakabali wa Taifa.

Jaji Mwambegele ameyasema hayo Juni 13, 2024 kwenye mkutano wa Tume na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam.

Advertisement

“Tunawasihi muendelee kutuunganisha na wadau. Tume itaendelea kuweka milango wazi kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara,” amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu kujiandikisha na umuhimu wake, hivyo Tume imejikita katika kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa ili uboreshaji uwe wa mafanikio.

Ameeleza kuwa Mifumo miwili itatumika ukiwemo wa (VRS) Mfumo Mkuu na (OVRS) ikiwa ni mfumo kwa njia ya mtandao.

Amesema mifumo yote miwili itahusisha fomu tatu, Namba moja, Kuandikisha wapiga kura wapya, Namba 5A wanaoboresha taarifa zao, wanaohama vituo, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, na namba 5B kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwepo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Uandikishaji wa wapiga kura utahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa Daftari wa mwaka 2024/2025 utatumia teknolojia ya BVR Kits zilizoboreshwa kwa kuwekewa program endeshi ya kisasa zaidi.

 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura utazinduliwa Julai 1, 2024 Mkoani Kigoma, mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.