INEC yaanza tena kuboresha daftari la kura

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa awamu ya pili utafanyika kuanzia leo hadi Julai 4, 2025.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele ambayo ilieleza kuwa awamu hiyo itakuwa na mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15 kwa wakati mmoja ndani ya siku saba kuanzia Mei Mosi hadi Mei 7, 2025 na vituo vya uandikishaji 3,808 vitatumika.

Alisema mikoa itakayohusika katika mzunguko wa kwanza ni Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe.

Jaji Mwambegele alieleza mzunguko wa pili utahusisha mikoa 16 kwa wakati mmoja na utafanyika kuanzia Mei 16 hadi Mei 22, 2025 ambapo vituo 3,921 vitatumika.

“Mikoa itakayohusika katika mzunguko wa pili ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma na Dar es Salaam. Mikoa mingine ni Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba,” alieleza.

Alisema mzunguko wa tatu utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye Magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 4, 2025.

Aliongeza kuwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Zanzibar ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vikiwa Tanzania Bara na vituo 210 vipo Zanzibar.

“Tunatarajia kuwa katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapigakura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapigakura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapigakura 148,624 watafutwa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye daftari,” alifafanua.

Vilevile, Jaji Mwambegele alikumbusha uboreshaji wa daftari hilo utahusisha kuandikisha wapigakura wapya wenye sifa na kutoa kadi mpya kwa wapigakura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika.

Pia, utatoa fursa kwa wapigakura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao, kuhamisha taarifa za wapigakura waliohama kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa taarifa za wapigakura waliopoteza sifa kwa sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button