INEC yaonya wanaojiandikisha mara mbili

Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Ramadhani Kailima.

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa onyo kwa wananchi wanaojiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti.

INEC imesema kwa watakaobainika adhabu yao itakuwa ni faini ya Sh 100,000-300,000 au kutumikia kifungo kwa muda usiopungua miezi sita na usiozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja.

Onyo hilo wamelitoa baada ya kubainika wako watu mkoani Dar es Salaam wamejiandikisha mara mbili na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Advertisement

“Kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114 (1) ch Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya Mwaka 2024 kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa la jinai,” alisema.

Aliongeza: “Adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha Shilingi 100,000 na isiyozidi Shilingi 300,000 au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani.”

Taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Ramadhani Kailima imesema mpiga kura atakayejiandikisha zaidi ya mara moja jina lake litafutwa katika vituo alivyojiandikisha na kuachwa katika kituo cha mwisho alichojiandikishia.

Alisema mpiga kura anaweza kukosa haki yake ya kupiga kura kama kituo hicho kinaweza kuwa si kituo chake sahihi anachopaswa kupiga kura.

Taarifa hiyo ilisema baada ya uchakataji wa taarifa katika daftari la wapiga kura kwa mfumo wa utambuzi wa alama za vidole kukamilika na waliojiandikisha zaidi ya mara moja kubainika orodha yao itakabidhiwa kwa jeshi la polisi kwa hatua za kisheria.

Kailima alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam uandikishaji unaendelea vizuri lakini kuna changamoto ya baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti.

Alisema baada ya uandikisha kukamilika tume italinganisha sura za watu wote waliopo kwenye daftari kupitia mfumo maalumu wa AFIS ili kubaini wapiga kura waliojiandikisha zaidi ya mara moja.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *