Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali kuendelea kufuatilia kwa karibu ili matengenezo ya injini mbili za ndege zilizoharibika yakamilike.
Aidha, Kamati hiyo imeitaka serikali kutathimini upya juu ya umiliki wa ndege zake kwa shirika la ndege la ATCL kuliko ilivyo sasa.
Akiwasilisha maoni juu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024, mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso ameitaka Serikali kulisaidia Shirika la ATCL ili kuweza kukabiliana na changamoto za madeni.
“Serikali iboreshe mafunzo ya kada ya marubani na wahandisi wa ndege ili kuongeza idadi yao hapa nchini,” amesema.
Awali, Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa amewasilisha mpango wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 huku akiliomba Bunge kuidhinisha takribani kiasi cha Sh trilioni 3.6 ili kuiwezesha Wizara kuifungua nchi kupitia barabara.
Katika hotuba yake aliyoiwasilisha Dodoma leo Jumatatu, Mei 22, 2023, Prof Mbarawa ameliaambia Bunge kuwa mbali na mambo mengine yatakayotekelezwa 2023/24, barabara saba zenye jumla ya urefu wa kilometa 2,035 zitaanza kujengwa kwa kiwango cha kupitia utaratibu wa EPC + F.