Iran kujadili nyuklia na nchi za Ulaya

IRAN : SERIKALI ya Iran imepanga kufanya mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia na Ufaransa, Uingereza na Ujerumani Januari 13, 2025, nchini Uswisi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa duru mpya ya mazungumzo kati ya Iran na mataifa matatu ya Ulaya yenye nguvu itafanyika mjini Geneva. Hata hivyo, alisisitiza kuwa mazungumzo hayo yatakuwa ni “mashauriano tu na wala sio majadiliano rasmi.”
Nchi hizo tatu za Ulaya zimeituhumu Iran kwa kuongeza hifadhi yake ya madini ya Urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha kutisha, bila sababu yoyote ya wazi inayohusiana na matumizi ya ndani.
Aidha, nchi hizo zimeonyesha uwezekano wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran ili kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kuendeleza mpango wake wa nyuklia. SOMA: Ulaya wahofia matumizi ya nyuklia
Mwanadiplomasia mkuu wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo “kwa njia ya haki na yenye heshima” na mataifa ya Magharibi.


