Iringa yavuta uwekezaji wa tril 20/-

MKOA wa Iringa umeendelea kupiga hatua kubwa katika kuvutia uwekezaji, huku takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zikionesha kuwa tangu mwaka 1997, umesajili miradi 241 yenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 8 sawa na zaidi ya Sh trilioni 20.

Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, alisema kuwa uwekezaji huu umejikita katika sekta za kilimo, viwanda, uchukuzi, na utalii, na umeweza kutengeneza ajira za kudumu zaidi ya 28,000.

Kwa mwaka wa fedha uliopita, Iringa ilisajili miradi mipya 12 yenye mtaji wa zaidi ya Dola milioni 61, sawa na zaidi ya Sh bilioni 152, na kuzalisha ajira 860.

Katika sekta ya kilimo, alisema mashamba makubwa yameanzishwa na viwanda vya kuchakata maziwa kutoka hali ya kimiminika hadi unga vimejengwa, na kuonyesha mchango mkubwa wa mkoa huu katika maendeleo ya kiuchumi nchini.

SOMA: TIC: Changamkieni fursa za uwekezaji

Kwa upande wa kitaifa, alisema mwaka wa fedha uliopita, Tanzania ilisajili miradi 707 ya uwekezaji, ikiwa ni ongezeko la asilimia 91 kutoka miradi 362 iliyosajiliwa mwaka uliotangulia.

Ongezeko hili lilihusiana na kuongezeka kwa mtaji wa uwekezaji kutoka dola bilioni 5.6 (Sh trilioni 14) hadi Dola bilioni 6.5 (Sh trilioni 16), huku ajira zikiongezeka kutoka 40,000 hadi zaidi ya 250,000.

Teri alifafanua kuwa ongezeko hili ni matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022, iliyowezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Alisema kwa mwaka wa kalenda wa 2024, TIC inalenga kusajili miradi 1,000 yenye thamani ya zaidi ya Dola bilioni 8.5, sawa na zaidi ya Sh trilioni 21, ambapo miradi ya zaidi ya Dola bilioni 5 inatarajiwa kutoka nje na Dola bilioni 3.5 kutoka kwa wawekezaji wa ndani.

“Hadi kufikia Juni 30 mwaka huu, tayari miradi 551 imesajiliwa, na hili linaonyesha kuwa lengo la kufikia miradi 1,000 ifikapo Desemba linawezekana,” alisema.

Teri alisema TIC inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki zaidi.

Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 2022 imeweka nafuu kwa wawekezaji wa ndani, ikihitajika kuwa na Dola 50,000 (Sh milioni 120) ikilinganishwa na Dola 500,000 (Sh bilioni 1.2) kwa wawekezaji wa nje.

SOMA: TIC yahimiza wawekezaji kusajili miradi yao

Alisema TIC pia imeanzisha dawati la pamoja linalojumuisha taasisi zote zinazohusika na masuala ya uwekezaji ili kuhakikisha changamoto zinazowakabili wawekezaji zinatatuliwa kwa haraka.

Teri aliupongeza mkoa wa Iringa kwa mchango wake katika kukuza uchumi wa Tanzania na kusema kuwa TIC itaendelea kuhamasisha uwekezaji zaidi ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Habari Zifananazo

Back to top button