ISRAEL: Baraza kupiga kura kusitisha mapigano Gaza

ISRAEL : WAZIRI Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema baraza lake la mawaziri halitakutana kuidhinisha mpango wa kusitisha mapigano na kuwaachia mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Ofisi ya Netanyahu imesema haitaidhinisha mpango huo hadi pale Hamas itakapoheshimu masharti yote yaliyokubaliwa.

Maafisa huko Gaza wamesema Israel imeendeleza mashambulizi yake katika Ukanda huo. SOMA: Viongozi wapongeza kusitishwa kwa mapigano Gaza

Hii ni baada ya wapatanishi hapo jana kuyatangaza makubaliano hayo wanayotumai yatapelekea kumalizika kwa vita vya Gaza.

Waziri mkuu wa Qatar ambaye ndiye mpatanishi mkuu, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim al-Thani amesema usitishaji huo wa mapigano utaanza kutekelezwa Jumapili na kuhusisha kubadilishana mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa tulipo leo, tunatumai huu ni ukurasa wa mwisho wa vita, na pande zote zimejitolea kutekeleza masharti yote ya makubaliano haya na zimejitolea kuendelea na hatua hizi kama ilivyoainishwa katika makubaliano haya,” amesema Thani.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezungumza na Rais wa Marekani Joe Biden na rais mteule Donald Trump, akiwashukuru kwa kusaidia kufikiwa makubaliano hayo.

Waandamanaji mjini Tel Aviv walishangilia wakati habari za makubaliano hayo zilipoanza kusambaa huku maelfu ya watu katika Ukanda wa Gaza wakiingia mitaani kushangilia pia.

Hamas imesema makubaliano hayo ni matokeo ya ujasiri wa Wapalestina na upinzani wao wa kishujaa katika Ukanda wa Gaza huku viongozi mbalimbali  duniani wakiponegza hatua hiyo.

 

Chanzo: Dw

Habari Zifananazo

Back to top button