ISRAEL: WAZIRI wa zamani wa Ulinzi nchini Israel, Yoav Gallant, aliyeondolewa madarakani mwezi Novemba baada ya kuongoza kampeni ya kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya mwaka mmoja, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya ubunge.
Gallant tayari ameshawasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Spika wa Bunge la Israel.
Amesema baada ya kuitumikia Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) kwa miaka 35 na zaidi ya muongo mmoja katika serikali na bunge, ni wakati sasa wa kutafuta mwelekeo mwingine.
“Kama ilivyo kwenye uwanja wa mapambano, ndivyo ilivyo katika huduma ya umma. Kuna wakati ambapo mtu lazima aache anachokifanya, aangalie upya na kuchukua mwelekeo mwingine ili kufikia malengo yanayohitajika. Njia ya Likud ndiyo njia yangu, naamini kanuni zake, na naamini wanachama wake na wapiga kura. Kama waziri wa zamani wa ulinzi, nawajibika kwa kila kitu kilichotokea mwanzoni mwa kazi yangu miezi kadhaa kabla ya kushika nafasi hii hadi mwisho wa kazi yangu,” alisema Gallant.
SOMA: Israel kukata rufaa dhidi ICC
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alimfuta kazi Gallant akisema hakuna uaminifu baada ya kutokubaliana katika masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na suala la kuingiza waumini wa Kiyahudi wa madhehebu ya Orthodox katika jeshi, hatua ambayo Netanyahu alipinga kwa kuhofia inaweza kuvunja serikali yake inayotegemea vyama vya kidini.
Mwezi Novemba, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa waranti ya kukamatwa kwa Netanyahu, Gallant, na kamanda wa kundi la Hamas, Mohammed Deif, kufuatia madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita kwenye Ukanda wa Gaza.