Israel yasitisha uhusiano UNRWA

ISRAEL : SERIKALI ya Israel imetangaza kusitisha uhusiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi wa Palestina UNRWA.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje imedai kuwa imeshatoa taarifa kwa Umoaj wa Mataifa kuhusu kusitisha uhusiano huo uliodumu muda mrefu kati ya Israel na UNRWA.
Hatua hii imekuja ikiwa ni mwendelezo wa sheria iliyopitishwa mwezi uliopita iliyotaka kuzuia shirika hilo kutofanya kazi nchini Israel.
Israel imedai kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi wa Palestina UNRWA limeingiliwa na wanamgambo wa Hamas jambo ambalo usalama wao uko hatarini.
Hatahivyo, Shirika la UNRWA limekanusha tuhuma hizo na kusema kuwa tangu kuanza kutoa huduma za kibinadamu katika ukanda wa Gaza, shirika hilo limekuwa likifuata miongozo ya kutoa huduma za kibinadamu kwa kila mtu bila ya ubaguzi .
Shirika la Umoja wa Mataifa –UN limesema uamuzi huo wa kusitisha uhusiano kutasababisha kudhorotesha shughuli za utoaji wa huduma za binadamu katika ukanda huo unaokabiliwa na vita vya muda mrefu.