Jaji Mkuu ahimiza tehama wadau wa mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ametoa wito kwa wadau wa mahakama kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika kazi zao ili kuendana na Mahakama ya Tanzania ambayo imeshaanza matumizi hayo na ifikapo mwaka 2025 kazi zake zote zitakuwa zikifanywa kwa mtandao.

Akizungumza na wadau wanaofanya kazi na mahakama wakati akihitimisha ziara ya wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani Songwe, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania haiwezi kuwa ya mtandao kama wadau wake hawataingia kwenye matumizi hayo kwa kuwa mnyororo wa upatikanaji wa haki unawahusisha wadau wote.

“Ukiiangalia ramani ya Mkoa wa Songwe utagundua kuwa kwa jinsi ilivyo, wananchi wengine wa mkoa huo watalazimika kufuata huduma za Mahakama kwa umbali mrefu hivyo Tehama ndiyo jibu”, alisema.

Advertisement

Alisema Mahakama ya Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya Tehama ambapo uwekezaji huo ukitumiwa vizuri utauwezesha mhimili huo kulingana na Mahakama nyingine duniani zenye maendeleo makubwa katika matumizi ya Tehama ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili za mkoa, wilaya za Mkoa wa Songwe, Jaji Mkuu aliwataka wajumbe hao kusimamia maadili na nidhamu ya mahakimu kwa kuwa wajumbe hao ni kiungo muhimu kati ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na wananchi.