DAR ES SALAAM :Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amezihimiza Taasisi zote nchini zinazotoa huduma kwa umma kuzingatia suala la haki na kuendelea kujitathimini juu ya huduma zinazotolewa kama zitaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050 ambayo inalenga kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na uchumi wa kipato cha kati.
Amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Kifamilia kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam kuelekea Maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria 2025 itakayofanyika kuanzia Januari 25 hadi Februari mosi kwa kuwaelimisha wananchi juu ya mambo mbalimbali ya kisheria katika maeneo yao.
Aidha Profesa Juma amewaomba waandishi wa habari nchini kuendelea kushirikiana na mahakama kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za mahakama kutokana na tathmini iliyofanywa kuonyesha wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha na hawaifahamu wiki ya sheria inayofanyika kila mwaka.
Wiki ya Sheria itafanyika jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Kikwete ambaye pamoja na mambo mengine ataongoza mbio za Hisani na Maadhimisho yatafungwa na Rais Samia Suluhu Hassan Februari 3 mwaka huu Dodoma.