‘Jamii irejeshe dhamana ulinzi wa mtoto kumkinga na ukatili’ 

ULINZI wa mtoto kwa jamii ya zamani ulikuwa shirikishi, yaani wa jamii nzima. Lakini hali hiyo sasa imebadilika jambo linalochochea kukua kwa vitendo vya ukatili kwa watoto.

Miongoni mwa maeneo yasio na ulinzi kwa watoto ni mazingira ya shule, kuanzia mtoto anapotoka nyumbani, kwenda shule na kurejea nyumbani. Hili limewaibua wadau wa ulinzi na usalama wa watoto Manispaa ya Shinyanga.

Wanasema maeneo ya shuleni hakuna mfumo rasmi wa ulinzi wa watoto hasa ambao hawawezi kujieleza vizuri.

Advertisement

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inaeleza umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza ni miaka minne hadi sita. Hapa ulinzi kwa watoto ni takwa la lazima.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwenge iliyopo Manispaa ya Shinyanga, Mika Paul anasema suala la mtoto kutoka nyumbani hadi shuleni katika suala la ulinzi na usalama wa mtoto mwalimu ni mlinzi wa kwanza maeneo ya shuleni.

Mwalimu Paul anasema walimu wamekuwa wakishinda na wanafunzi hao muda mrefu ila usalama katika safari ya kuja shule na kurudi nyumbani ni jukumu la jamii nzima.

Anasema shule hiyo imekusanya watoto takribani kutoka kata zote za manispaa na kuna watoto wa darasa la awali na la kwanza zaidi ya 400 baadhi yao wanatoka mbali wanalazimika kutembea umbali wa kilometa tatu hadi nne.

Mwalimu Paul anasema usalama wa watoto katika kusafiri kutoka shule kwenda nyumbani ni changamoto kwani wazazi wengi wanatumia usafiri wa baiskeli au bodaboda kwa kuwaamini madereva hao.

“Wazazi wengi wamekuwa wakiwaamini madereva bodaboda na baiskeli kuwa ndio watakuwa wanawafuata watoto wao wawapo shuleni bila kuwashirikisha walimu matokeo yake hawawafikishi nyumbani kwa wakati,” anasema Mwalimu Paul.

Anasema wakati mwingine bodaboda hao hawafiki shule kwa wakati kuwachukua watoto na kusababisha mtoto aanze kutembea kwa miguu kurudi nyumbani umbali wa kilometa sita na mara nyingi hujikuta wakipotea.

“Nimekuwa nikipata kesi nyingi, juzi kuna mtoto wa miaka mitano wa darasa la awali alipotea nakuja kupatikana saa nne usiku, kilichosababisha ni dereva wa baiskeli aliyetakiwa kumfuata kila siku hakutokea,” anasema Mwalimu Paul.

Anasema mzazi wa mtoto huyo alifika mpaka kituo cha polisi kutoa taarifa mtoto wake kapotea akiwa shuleni. Hata hivyo, walionywa kuacha kuwaamini madereva wa baiskeli au bodaboda pekee bali waanze na walimu kulinda ulinzi wa watoto.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mitimirefu, Kata ya Mjini, Manispaa ya Shinyanga, Nassor Warioba, anasema suala la ulinzi na usalama wa mtoto linafanyiwa mipango mikakati ya namna ya kuwadhibiti madereva bodaboda au baiskeli wanaobeba wanafunzi.

Warioba ataja mipango ni pamoja na kujenga uzio katika shule ili kila mwendesha baiskeli na bodaboda akimfuata mtoto asaini kwenye kitabu na kuonesha tarehe na muda aliomchukua mtoto kuimarisha ulinzi na usalama mzuri wa mtoto kufika salama nyumbani.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Kata ya Mjini, Blandina Mwinamila anasema   wazazi wamekuwa wakiamini madereva wa bodaboda na baiskeli ambao kimyakimya wamekuwa wakiwafanyia vitendo vibaya watoto na kuwapa vitisho.

Mwinamila alitoa ushauri kwa walimu kwamba watoe elimu kwa wazazi na waendesha bodaboda wanaowachukua wanafunzi shuleni kuhusu ulinzi na usalama wa watoto na adhabu kali kwa watakaowanyanyasa watoto.

Ofisa huyo anasema hushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa hutoa elimu kwa wazazi ili kuondoa changamoto ambazo watoto hawawezi kuzieleza sababu ya vitisho.

Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo anasema ukatili unaofanywa kwa watoto walio chini ya miaka minane umekuwa wa kimyakimya na wanabaki na maumivu mwilini tofauti na watoto wenye umri wa kuanzia miaka 10 wakifanyiwa ukatili wanasema.

“Ukatili unaofanywa kwa watoto kimyakimya umetukosesha kuujua kwa urahisi na kupata takwimu zao ukilinganisha na takwimu za watoto walio zaidi ya miaka kumi,” anasema Mweyo.

Kwa upande wake, Ofisa wa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Tedson Ngwale, anasema asilimia 40 ya watoto hufanyiwa ukatili katika mazingira ya shule (njiani) na asilimia 60 ni nyumbani.

Wazazi wenye watoto wanaosoma Shule ya Msingi Mwenge, Juliana Selestine na Adamu David, kwa nyakati tofauti wanasema watoto kufuatwa na baiskeli au bodaboda (zinazoitwa daladala) si jambo baya kwa kuwa wengi wa madereva ni waaminifu lakini ni ukweli kuna ambao si waaminifu.

David anasema ukatili kwa watoto unachangiwa na wazazi wasiowalipa madereva fedha za usafiri wanazokubaliana na kuamua kumalizia hasira kwa mtoto jambo lisilokubalika.

Madereva wa bodaboda na baiskeli Manispaa ya Shinyanga, Magadula James na Salum Rashid, wanasema wapo madereva wengine wamekuwa na tabia mbaya za kuwafanyia watoto ukatili lakini si wote.

Magadula anasema yeye anafahamu kuwa dhamana ya usalama wa mtoto anapokabidhiwa ili ampeleke shule au kumrejesha nyumbani ni juu yake.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 kila mtoto
anayo haki ya kuishi na kupata malezi bora, ulinzi na anapokuwa nyumbani au kwenye jamii anapaswa kulindwa dhidi ya matukio ya ukatili na kuhakikishiwa usalama wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi anasema suala la ulinzi na usalama kwa watoto ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha watoto wanakuwa kwenye mikono salama.

Takwimu za Jeshi la Polisi za mwaka 2021 zinaonesha matukio ya ukatili kwa watoto yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi ni 11,499. Mikoa inayoongoza kwa ukatili ni Arusha (808), Tanga (691) na Shinyanga (505).

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *