NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis ameitaka jamii kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya kutunza na kuhifadhi mazingira ili kuwa na kizazi chenye uelewa na kuthamini mazingira hususan uchumi wa bluu.
Ametoa rai hiyo wakati wa ufunguzi wa warsha ya Kimataifa wa Jumuiya ya Ukanda wa Bahari ya Hindi (IORA) jijini Dar es Salaam iliyoratibiwa na Chuo Kikuu Mzumbe, Wizara ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kushirikisha nchi zinazozunguka ukanda wa Bahari ya Hindi.
Naibu Waziri Khamis ametoa rai kwa wadau wote wa IORA, kuhakikisha kwamba jamii inapata uelewa na elimu sahihi ya kuhusu utunzaji wa Mazingira.
SOMA: ‘Wananchi zingatieni utunzaji Mazingira’
“Sisi wasomi twendeni tukatoe elimu kwa jamii kuhusu kutunza Mazingira, jamii yetu haina uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya Ikolojia, kaboni na namna bora ya utunzaji wa mazingira twende tukawaelimishe watu jinsi ya kuvuna kaboni” amesisitiza Khamis.
Amesema uelewa wa masuala ya Kaboni na matumizi sahihi ya rasilimali za bahari kupitia uchumi wa bluu ni muhimu kwa jamii inayozunguka mazingira ya pwani kwa kuwa husaidia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kutoa rai kwa Jumuiya ya Ukanda wa Bahari ya Hindi kuweka nguvu zaidi katika kutoa elimu ya matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, amesema wakati ni sasa wa kuunganisha nguvu za wasomi, watafiti na wanamazingira kuendelea kuhimiza uhifadhi wa mazingira na kusisitiza matumizi sahihi ya uchumi wa bluu kama njia ya kulinda mazingira na chanzo cha maendeleo endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema nchi au ukanda wa IORA umeanza kugundua na kutumia faida za uchumi wa buluu katika juhudi za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa njia endelevu.