Jamii yahimizwa kuwekeza mustakabali wa watoto

DAR ES SALAAM: Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, wadau wa maendeleo ya watoto wameitaka jamii na serikali kuongeza uwekezaji katika malezi, afya, elimu na huduma za maji safi ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye kuwajengea mustakabali bora.

Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka kuenzi kumbukumbu ya watoto wa Soweto nchini Afrika Kusini waliouawa mwaka 1976 walipokuwa wakidai haki ya kupata elimu bora. Miaka 50 baadaye, swali linaendelea kubaki; je, watoto wa Afrika wanapata mazingira stahiki ya kukua, kujifunza na kustawi?

Mwaka 2026, Tanzania inaadhimisha siku hiyo chini ya kaulimbiu isemayo “Malezi ya Mtoto ni Msingi wa Familia Bora na Taifa Imara,” huku kaulimbiu ya Umoja wa Afrika ikiwa “Kuhakikisha Upatikanaji wa Huduma za Maji Safi, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi kwa Kila Mtoto Barani Afrika.”

Akizungumza na Habari leo wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja wa Mawasiliano na Uchechemuzi wa Shirika la Save the Children Tanzania, Victoria Marijani, alisema malezi bora huanza tangu mtoto akiwa tumboni kwa mama.

“Malezi siyo tu kumlisha mtoto. Ni mchakato unaoanza tangu ujauzito. Mtoto anapopata lishe bora tumboni, upendo baada ya kuzaliwa, mazingira salama na msisimko wa kujifunza katika miaka mitano ya kwanza ya maisha, ubongo wake hukua kwa kasi kubwa. Miaka hii ndiyo msingi wa afya, tabia na uwezo wa kujifunza katika maisha yake yote,” amesema Victoria.

Ameongeza kuwa familia ndiyo mwalimu wa kwanza wa mtoto, lakini haiwezi kufanya kazi hiyo peke yake bila msaada wa jamii, shule salama, vituo vya afya na sera rafiki zinazolinda haki za watoto.

Kwa mujibu wa Victoria, mtoto anayelelewa katika mazingira ya upendo, usalama na huduma bora ana nafasi kubwa ya kuwa raia mwenye afya njema, elimu bora na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia suala la maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi, alisema bado watoto wengi nchini wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa maji salama na miundombinu bora ya usafi.

“Takwimu na uzoefu wetu vinaonesha kuwa shule na jamii nyingi bado zinakosa maji ya uhakika. Watoto hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji badala ya kusoma.

Wengine hunywa maji yasiyo salama na kuugua magonjwa kama kuharisha na kipindupindu, hali inayochangia utoro na kudhoofisha maendeleo yao ya kielimu,” amesema.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa vyoo bora na salama, hususan kwa wanafunzi wa kike wanaohitaji mazingira yenye faragha wakati wa hedhi.

Mwalimu Mwandamizi wa Shule ya Sekondari Temeke anayesimamia Malezi na Nidhamu, Roman Kitali, alisema baadhi ya shule bado zinakabiliwa na changamoto kubwa za usafi.

“Katika baadhi ya shule unakuta mwanafunzi anavua shati na kuliacha nje kabla ya kuingia chooni ili asibebe harufu ya chooni darasani kwa kuhofia kuchekwa na wenzake. Hili ni tatizo linaloathiri ustawi na mwenendo wa masomo ya wanafunzi,” amesema Kitali.

Wadau hao wanasema gharama za kutowekeza katika huduma za usafi na vyoo bora ni kubwa zaidi kuliko gharama za kuzijenga, kwa kuwa magonjwa yanayozuilika husababisha familia kutumia fedha nyingi kwa matibabu huku watoto wakipoteza muda wa masomo.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Sydney Mdoe, alisema taasisi hiyo imeendelea kutoa kipaumbele kwa upatikanaji wa maji katika shule, hospitali na taasisi nyingine za umma.

“Tunafanya kila jitihada kuhakikisha shule na taasisi za umma zinapata huduma ya maji wakati wote. Hata pale ambapo kuna changamoto za bili, kipaumbele chetu ni kuhakikisha wanafunzi na wananchi wanaendelea kupata maji safi na salama,” amesema Mdoe.

Amesema Serikali imefikia zaidi ya asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini na inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kila kijiji kinapata huduma hiyo ndani ya umbali usiozidi mita 400 kutoka kwa mtumiaji.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Vaileth Mulyalya, alisema wizara imeendelea kutoa elimu ya malezi na afya ya mtoto, ikiwamo masuala ya usafi binafsi.

“Tumeandaa miongozo na vitini vya kufundishia malezi ya watoto ambapo afya na usafi ni miongoni mwa mada muhimu zinazotolewa kwa wazazi na walezi,” amesema.

Wadau hao wameeleza kuwa uwekezaji katika maji safi, vyoo bora, malezi na ulinzi wa mtoto ni msingi wa kujenga taifa lenye wananchi wenye afya, elimu na uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi.

“Watoto wa leo ndiyo Tanzania ya mwaka 2040. Tukiwapa maji safi, malezi bora na mazingira salama leo, tutakuwa tumejenga msingi wa taifa imara la kesho,” wamesisitiza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button