Japan kutoa tril 70/- za miradi, mazingira Afrika

SERIKALI ya Japan imeahidi kutoa dola za Marekani bilioni 30 (sawa na Ths 69.9 za Tanzania ) kuziwezesha nchi za Afrika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuimarisha utunzaji wa mazingira.

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida alitoa ahadi hiyo Jumapili wakati akitoa hotuba kwenye mkutano wa nane wa kimataifa wa wakuu wa nchi na serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD8) unaofanyika jijini Tunis nchini Tunisia.

Akizungumza kwa njia ya mitandao wakuu hao kwenye ukumbi wa Palais des Congres, jijini Tunis,Kishida alisema fedha hizo zitatolewa kwa kipindi cha miaka mitatu ili kuimarisha utunzaji wa mazingira, uwekezaji hasa kwa vijana, sekta za afya, viwanda na elimu.

“Ijapokuwa siko pamoja nanyi kwenye mkutano huo, bado dhamiri yangu ya kuendeleza bara la Afrika iko palepale, haijabadilika. Kwa kuanzia, Japan itaanzisha “Japan’s Green Growth Initiative with Africa” ambapo itatoa dola za Marekani bilioni nne kwa taasisi za umma na za binafsi barani Afrika ili kuziwezesha kutekeleza mpango huo,” alisema.

Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa Japan imelenga kukuza uwekezaji na sasa wamelenga kuwainua vijana wanaoanzisha kampuni ili vijana wa Afrika na wa Japan wafanye kazi kwa karibu.

Kuhusu kuboresha maisha ya Waafrika, Kishida alisema kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) watatoa dola za Marekani bilioni tano zinazojumuisha mkopo mpya wa dola za Marekani bilioni moja zinazolenga kuzisaidia nchi hizo kumudu madeni.

Alisema kujitokeza kwa janga la corona kumetoa funzo kuwa kuna haja ya kujiandaa kukabil magonjwa ya mlipuko na kwa kuzingatia hilo, Serikali ya Japan itachangia dola za Marekani bilioni 1.08 ili kuiwezesha Afrika kukabili UKIMWI, kifua kikuu, malaria na kuimarisha mifumo ya afya.

“Vilevile, tutaimarisha rasilmali watu kwa kuwajengea uwezo wataalamu barani Afrika. Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, Japan inatarajia kuwajengea uwezo zaidi ya watu 300,000 kutoka bara la Afrika katika sekta za viwanda, afya, utabibu, elimu, kilimo, sheria na utawala.”alisema Kishida.

Kuhusu kilimo, alisema hivi karibuni Japan kwa kushirikiana na AfDB imeamua kutoa dola za marekani milioni 300 ili kuzisaidia nchi za Afrika kuzalisha chakula kwa wingi na kuwajengea uwezo watu 200,000 walioko kwenye sekta ya kilimo.

“Aidha watatoa msaada wa chakula wenye thamani ya dola za marekani milioni 130 ili kuzisaidia nchi hiyo kukabiliana na upungufu wa chakula.”ilieleza taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Mapema, akifungua mkutano huo, Rais wa Tunisia, Kais Saied ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano wa TICAD 8 alisema nchi za Afrika zina rasilimali nyingi lakini watu wake bado wanakabiliwa na umasikini.

Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Macky Sall alisema bara la Afrika linahitaji kuwezeshwa kuwa na nishati ya uhakika ili lizalishe bidhaa zake.

“Tunahitaji kuona nchi za Kiafrika zikizalisha mbolea ya kutosha ili tuwe na uhakika wa kilimo, kwa hiyo tunakaribisha wabia kutoka Japan katika sekta hii muhimu ya uzalishaji katika nchi nyingi,” alisema.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button