Jela miaka 30 unyang’anyaji kutumia silaha
MKAZI wa kijiji cha Bugolola wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, John Chibuga ,31, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe, Lucas Nyahega ambapo amesema kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Mahakama imejiridhisha pasi na shaka kwamba mshtakiwa ametenda kosa hilo.
Awali, akisoma shtaka hilo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Aidan Nziku alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 15, 2023 saa 14:00 mchana katika kijiji cha Kakerege Wilaya ya Ukerewe kwa kumvamia Mdala Mangu( 34) akiwa nyumbani kwake na kumkata na panga sehemu mbalimbali ya mwili wake kisha kuiba simu ya mkononi na kukimbia kinyume na kifungu namba 287A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura 16 toleo la mwaka 2022.
Hata hivyo, mshitakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu kutokana na shtaka linalomkabili, aliomba mahakama impunguzia adhabu kwa sababu alikuwa hana pesa ya kujikimu baada ya kutoka gerezani ndio akaamua kwenda kupora.
Aidha, mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa ni mtenda kosa wa mara ya pili na aliachiliwa huru kwa msamaha wa Rais Desemba 9, 2023 kwa kosa la kuvunja duka usiku na kuiba ambapo alitiwa hatiani na mahakama ya Mwanzo Nansio na Desemba 15, 2023 akarudia kosa.



