Jenereta za kuzalisha umeme Kigoma kuzimwa Sept.30

KIGOMA;  SHIRIKA la Umeme (TANESCO) limesema kuwa litazima  umeme unaozalishwa kwa kutumia mashine za mafuta ifikapo Septemba 30 mwaka huu, ili kuwezesha kuanza rasmi kwa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa kwa wilaya zote za Mkoa Kigoma Oktoba Mosi waka huu.

Meneja wa mradi wa kusafirisha umeme kutoka kituo cha Nyakanazi Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kwenda mkoani Kigoma urefu wa kilometa 280, Mhandisi Baraka Magogw,  alisema hayo wakati waandishi wa habari walipofanya ziara kutembelea utekelezaji wa mradi na kwamba kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 80.

Mhandisi Baraka Magogwa

Magogwa amesema kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya kiasi cha Sh Bilioni 434.9 unahusisha miradi mitatu ndani yake, ikiwemo ujenzi wa njia ya kusafirisha wa umeme msongo wa Kilovolt 400 kutoka Nyakanazi Kwenda kituo cha kupokea umeme kinachojengwa Kidahwe nje kidogo ya mji wa Kigoma.

Akieleza utekelezaji wa miradi hiyo, Mhandisi wa miradi hiyo kutoka TANESCO Kigoma, Mhandisi Nyango Magessa amesema kuwa ukiacha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pia wanatekeleza mradi wa ujenzi wa kituo kidogo cha kupokea umeme wa msongo wa kilovolt 220 eneo la Kidahwe, ili kuwezesha umeme wa gridi kuanza kutumika kuanzia Oktoba Mosi mwaka wakati ujenzi wa kituo kikubwa cha kupokea umeme wa msongo wa Kilovolt 400 ukiwa ndiyo ukianza.

Mhandisi Magessa amesema kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi kuja mkoani Kigoma unaotekelezwa na Kampuni ya M/s TATA project Ltd ya India kwa gharama ya shilingi Bilioni 185.7, umefikia asilimia 95 na kwamba kwa kazi ya utekelezaji wa mradi ulivyo wana hakika umeme utaanza kutumika kufikia wakati huo.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unatoa uhakika kwa serikali ya mkoa na serikali kuu kutekeleza kwa vitendo maono ya Raisi Samia Suluhu Hassan ya kuufanya mkoa Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati kiuchumi na biashara

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaiwezesha serikali kuepuka gharama kubwa inayotumika  sasa kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta kiasi cha Sh 1000 kwa uniti moja huku umeme huo ukiuzwa kwa wananchi kwa shilingi 100 kwa Unit moja.

Habari Zifananazo

Back to top button