Jengeni mazoea kupima udongo wa kilimo

WAKULIMA wameshauriwa kujenga mazoea ya kupima udongo kabla ya kulima, ili kujua virutubisho vilivyopo kwenye udongo ambavyo vitawasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina ya mazao yanayofaa kupandwa.
Mkuu wa Maabara ya Sayansi za Udongo kutoka Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia iliyopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Amour Suleiman ametoa ushauri huo Agosti 3, 2023 katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro.
Suleiman amesema pamoja na kupima udongo, pia mkulima anapaswa kujua aina ya virutubisho vilivyopo kwenye mbolea atakayoitumia, pamoja na kiwango kinachohitajika kwenye udongo, kwani sio kila mbolea inatumika kwenye kila udongo.

“Tunawakaribisha kwenye banda letu hapa mtaweza kujionea teknolojia ambazo tunazo na za kisasa zaidi tunazotumia katika upimaji wa sampuli zetu, tunatoa huduma ya kupima bure udongo na maji na kutoa majibu kwenye banda letu, lakini ni kwa baadhi tu ya vipimo , si vipimo vyote ambavyo tunaweza kupima kwenye banda ,” amesema Suleiman.
Katika hatua nyingine ameshauri wakulima wanaotumia maji ya visima kumwagilia mashamba yao kuhakikisha maji hayo yanapimwa, ili kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Kumwagilia maji ya kisima yasiyopimwa kunaweza kusababisha kuweka tatizo ambalo halikuwepo katika udongo wako,” amesema Suleiman na kuongeza:
“ Unaweza kukuta maji yana chumvi kali sana ukakuta unahamishia ile chumvi kwenye udongo na udongo wako usiweze kufaa tena kwa matumizi ya kilimo, kwa sababu kuja kuurudisha kwenye hali yake ya kawaida itakugharimu kwa kiasi kikubwa, ” amesema Suleiman.



