Jenista ashitukia mfumo Tehama hospitali ya rufaa

WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Seif Shekalage kutuma timu ya wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kufanya ukaguzi na kuangalia kama mfumo wa Tehama unafanya kazi ipasavyo.

Jenista alitoa maagizo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu katika hospitali hiyo kisha kuzungumza na watumishi.

Alisema mfumo wa Tehama kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa utoaji huduma bora za afya kwa wananchi, ikiwemo kuweka ulinzi na usalama wa miundombinu ya hospitali.

Alisema alipewa taarifa na uongozi wa hospitali hiyo kuwa wamekuwa wakitumia walinzi kufuatilia upotevu wa baadhi ya vitu, utaratibu ambao alisema umepitwa na wakati kwani kila kitu kinaendeshwa kwa Tehama.

“Hospitali hii imewekwa mifumo ya Tehama, kama mfumo wetu umeunganishwa idara zote za hospitali inakuwaje tushindwe kudhibiti mwenendo mzima wa shughuli zote zinazofanyika kwenye hospitali yetu?” alihoji.

Alisema inawezekana kwenye hospitali hiyo kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakichezea mfumo au una matatizo ambapo ameagiza uongozi kufanyia kazi jambo hilo.

Katika hatua nyingine, ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa huduma bora ambazo wamekuwa wakizitoa kwa wananchi, ikiwemo suala la usafi kwenye hospitali.

Awali, akitoa taarifa ya hali ya afya ya mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Boniphace Marwa alishukuru serikali kwa kuleta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya afya ambayo imeboresha utoaji wa huduma.

Dk Chacha alisema kuwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa, wanakabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa. Alimuomba Jenista kuwaongezea wataalamu ili huduma zote za kibingwa ziweze kutolewa kwenye hospitali hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button