CHAMA cha Waandishi wa Habari Mazingira Tanzania (JET) kimetoa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuandika habari za masuala ya uhifadhi wa ukanda hasa kupambana na uhalifu haramu wa Misitu na kupambana na uhalifu wa wanyamapori.
Mafunzo hayo pia yamelenga kujenga uelewa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, jinsia na uhifadhi wa bioanuwai.
Mkurugenzi wa JET ,John Chikomo ameiabia habariLEO kuwa mafunzo hayo yatahusisha waandishi 20 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania ambayo yatafanyika Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Bagamoyo Februari 15 na 16,2024.
“Mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya tuhifadhi Maliasili (“Hifadhi Maliasili”) mradi unaoungwa mkono na USAID utakaofanyika kwa miaka mitano na inashughulikia tishio,harakati za wanyama na bioanuwai nchini Tanzania.
Chikomo amesema kupitia mafunzo hayo waandishi wa habari watakuwa na ujuzi sahihi, mtazamo wa kuwa na uwezo wa kufanya taarifa za uchunguzi juu ya uhifadhi wa bioanuwai na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema wanahabari wanatarajiwa kupata uwezo na maarifa ya masuala ya uhifadhi ili kuchunguza, kuripoti na kuchambua kwa ufanisi na uhifadhi wa baharini na misitu, usafirishaji naujangili, na kukuza uhifadhi wa wanyamapori na masuala ya utalii.
Chikomo amesema mbali na kutengeneza mitandao kwa kuwaunganisha waandishi wa habari na wadau wa uhifadhi katika ngazi mbalimbali, waandishi wataboresha ubora wa habari zao.
“Mradi wa ‘USAID Tuhifadhi Maliasili’ ina afua katika ukanda wa wanyamapori kama vile mfumo wa ikolojia ya shoroba ya kwakuchinja inayounganisha Tarangire-Manyara katika Wilaya za Babati na Monduli, mikoa ya Manyara na Arusha, Ushoroba wa Kigosi Moyowosi-Burigi Chato- unaounganisha Kigosi Moyowosi Complex na Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato ulioko Biharamulo na Kakonko Mkoa wa Kagera na Kigoma.
Amesema maeneo mengine ni ushoroba wa Nyerere Selous-Udzungwa inayounganisha Nyerere Selous na hifadhi za Taifa za Milima ya Udzungwa katika Mji wa Ifakara, Mkoa wa Morogoro, Ushoroba wa Hifadhi ya Mazingira ya Amani na Nilo inayounganisha Hifadhi ya Msitu wa Mazingira katika Wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga.
“Ushoroba wa Ruaha Rungwa-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha,pori la Akiba la Rungwa, Mapori ya Akiba ya Lukwati na Pigi, na Katavi Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya,Ushoroba wa Ruaha Rungwa-Inyonga unaounganisha hifadhi ya taifa ya Ruaha Taifa na Mapori ya Akiba ya Rungwa na Inyonga Itigi wilaya ya Sikonge , Mikoa ya Singida na Tabora.
Mengine ni ushoroba wa Mahale-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale na Katavi Complex katika Wilaya za Tanganyika na Uvinza, Katavi na mikoa ya Kigoma.