JK ashauri bei umeme, gesi kuangaliwa
DAR ES SALAAM – RAIS wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ameshauri ili kufanikisha azma ya nishati safi ya kupikia kuwafikia wananchi wengi ni vyema bei ya umeme ikapungua.
Alisema hayo jana alipotembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba.
Akizungumza akiwa kwenye banda ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), aliwapongeza kwa kazi kubwa wanayofanya kusambaza umeme vijijini na kusema wakati anaingia madarakani chini ya asilimia 10 ya wananchi wa vijijini ndio walikuwa na umeme.
“Leo zaidi ya vijiji 12,031 vimeunganishwa umeme vijijini zaidi ya asilimia 98, vilivyobaki ni vijijini 207 tu,” alisema Kikwete.
Alisema kwa idadi hiyo ni wazi wananchi wengi vijijini wameunganishwa umeme na hivyo kufanya watumiaji wa umeme nchini kuongezeka na kuwa iwapo bei ya umeme itapungua itawafanya wananchi wengi zaidi kutumia nishati hiyo kupikia kwa sababu kuna majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo.
“Tuangalie Tanesco wakipunguza bei ya umeme wananchi wengi wataweza kuitumia kama nishati safi ya kupikia, sasa hivi mkaa na kuni ndio wapinzani wakubwa wa umeme na miti inakatwa kwelikweli, tunaharibu mazingira, hatupandi miti,” alisema Kikwete.
SOMA: Serikali yapongeza wadau nishati ya kupikia
Alitoa mfano kuwa miaka kadhaa iliyopita akiwa nyumbani kwake Msoga, Pwani alikuwa hawezi kuona hata magari yakipita Chalinze kwa sababu ya misitu ya miti, lakini sasa anaweza hata kuhesabu idadi yake.
Aidha, aliwataka wauza gesi ya kupikia wasiwe na tamaa kupandisha bei ili wananchi wengi pia waweze kuitumia kupikia.
Alisema nishati ya umeme si kwa ajili ya kupikia tu ikiwepo na kuwafikia wananchi wengi wataitumia katika shughuli za uzalishaji mali. Akizungumzia maonesho hayo, alisema yameboreshwa na hata bidhaa zimeongezwa ubora.