Serikali yapongeza wadau nishati ya kupikia

DAR ES SALAAM – Serikali imepongeza juhudi za washirika wa maendeleo ukiwemo Umoja wa Ulaya (EU) katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia, mkakati mahususi wa Rais Samia Samia Suluhu Hassan kuwezesha taifa kuwa na nishati safi majumbani.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema wakati akifungua Waarsha ya Nishati Safi ya Kupikia iliyoanza leo Juni 19 jijini Dar es Salaam kuwa serikali inatambua michango ya wadau wa maendeleo.
“Kuna programu mbalimbali zinazotekelezwa na washirika wa maendeleo na sekta binafsi ikiwemo ya mradi wa CookFund unaoendelea katika nchi yetu,” amesema “tuko tayari kuendelea kushirikiana na UNCDF na wadau wengine wa nishati safi ya kupikia.”
Kapinga amewataka wadau kushirikiana na serikali ili kwa pamoja kutafuta na kupendekeza mikakati ambayo itaharakisha lengo la nchi kufikia asilimia 80 ya watanzania kutumia Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.
“Warsha hii ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia wakati akizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi 2024 – 2034, ambapo aliagiza Wizara ya Nishati kukaa pamoja na wadau kutekeleza malengo ya mkakati huo,” amesema Kapinga.
SOMA: Rais Samia akiwasili Jengo la Umoja
Serikali imewataka wadau kuwa wabunifu, kuonesha juhudi na kudumusha ushirikiano miongoni mwa wadau wa sekta ili kufikia lengo.
Naibu Waziri amesisitiza kuwa Serikali itaweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kila kaya ili kuimarisha afya ya umma na maendeleo endelevu katika Sekta ya mazingira na uchumi.
Mkuu wa Shirika la UNCDF nchini, Peter Malika amesema wanashirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali ikiwemo mfuko wa CookFund unaolenga kuimarisha Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema Nishati Safi ni fursa na biashara ambapo aliwataka wadau mbalimbali kuichangamkia fursa hiyo kwa sasa.
Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo Watunga Sera, Wadau wa Maendeleo, Wabunifu, Sekta Binafsi na Washirika wa Kimataifa.