JK: Wanafunzi wafaidike na tafiti zao

DAR ES SALAAM: RAIS Mstaafu, Jakaya Kikwete ametoa wito kwa mamlaka za elimu ya juu nchini kuhakikisha tafiti wanazofanya wanafunzi vyuoni ziwe na manufaa kwao na jamii ili tija ya elimu yao iweze kuonekana.

Mkuu huyo wa nchi wa Awamu ya Nne amesema hayo leo Julai 06, 2024 alipotembelea Banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ndani ya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba 2024) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha mahudhurio UDSM

“Tafiti hizi hazipaswi kuishia pale tu unapovalishwa joho na kutunukiwa shahada, ila inapaswa kuwe na namna ya ‘ku-commercilize’,” amesema Dk. Kikwete.

SOMA: Sh bilioni 1 kutumika kwenye tafiti

Pia, Mzee Kikwete ameeleza kufurahishwa namna Sabasaba ya mwaka huu kuonekana kuwa bora kuliko miaka iliyopita.

Ametaja miundombinu rafiki kama barabara za lami kuwa ni miongoni mwa yaliyomvutia katika maonesho ya mwaka huu.

Katika ziara yake ndani ya Sabasaba 2024, Kikwete ametembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Banda la Zanzibar ambapo amejionea bidhaa mbalimbali ikiwemo zile zinazotokana na Uchumi wa Buluu.

Pia, Mkuu huyo wa UDSM, ametembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo amejionea vivutio mbalimbali vikiwemo, bidhaa za asili ikiwemo asali, nguo za vitenge, batiki, vinyago, vyungu, wanyama na ndege pori kama chui, pundamilia, nyani, tausi, kasuku na wengineo.

Hata hivyo, katika ziara hiyo ameisihi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuhakikisha wanaboresha muonekano wa maelezo ya wanyama katika mabango yao ili yaweze kusomeka kiwepesi na kuwanufaisha watalii wa ndani hata wa nje.

Ikumbukwe, mnamo Septemba 02, 2023 Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ilitoa Sh. bilioni 1.29 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi saba ya kitafiti kutoka katika taasisi mbalimbali hapa nchini.

Baadhi ya maeneo yaliyonufaika na fedha hizi ni kuwa ni  Uanzishwaji wa Vigoda viwili vya utafiti katika chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha na Tathmini ya madhara ya COVID19 kupitia MUHAS, UDOM.

Sabasaba 2024 imezinduliwa rasmi na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi sanjari na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Julai 04, mwaka huu akiwa katika ziara ya kikazi nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button