JKCI Dar Group yaongeza huduma tatu mpya za moyo

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, kwa kipindi cha mwaka mmoja, imeanzisha huduma tatu mpya za matibabu ya moyo na mishipa ili kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Huduma hizo ni kipimo cha kufuatilia shinikizo la damu kwa saa 24, kipimo cha kuangalia umeme wa moyo kwa saa 24, pamoja na kipimo cha kuchunguza mishipa ya damu ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wakati wa mazoezi kwa kutumia mashine ya treadmill.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Dk. Tulizo Shemu, amesema hospitali hiyo ilitoa huduma za upimaji na matibabu kwa wagonjwa 138,699 kwa mwaka 2025. Kati yao, watu wazima walikuwa 124,959 na watoto 13,740. Wagonjwa waliolazwa walikuwa 4,144, wakiwemo watu wazima 3,031 na watoto 1,113.

Amesema ukilinganisha na mwaka 2024 ambapo hospitali ilihudumia wagonjwa 133,756, kumekuwa na ongezeko la wagonjwa 4,943. Hata hivyo, idadi ya watoto imepungua huku idadi ya wagonjwa watu wazima ikiongezeka.

Dk. Shemu ameongeza kuwa hospitali hiyo hutoa huduma mbalimbali zikiwemo matibabu ya magonjwa ya moyo, kinywa na meno, ngozi, magonjwa ya kuambukiza ikiwemo malaria, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na wajawazito, huduma za macho pamoja na kliniki ya pua, masikio na koo.

Huduma nyingine zinazotolewa ni pamoja na matibabu ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya tumbo na ini, figo, upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za mazoezi tiba pamoja na huduma za maabara. SOMA: JKCI yatoa mil 200/- kwa mwezi msamaha wagonjwa wa moyo

Kuhusu huduma za tiba mkoba kupitia mpango wa Samia Suluhu Hassan Outreach Services, Dk. Shemu amesema huduma hizo zilitolewa kwa wananchi wa Mbagala wilayani Temeke, ambapo jumla ya wananchi 251 walipatiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo, ngiri, vidonda sugu, matatizo ya mifupa na mgongo pamoja na huduma za kinywa na meno.

Amesema katika kambi hiyo, watu 198 walibainika kuwa na magonjwa mbalimbali na kupewa rufaa ya kufika hospitalini hapo kwa vipimo zaidi na kuanzishiwa matibabu. Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, wagonjwa 1,874 walifanyiwa upasuaji wa aina mbalimbali ikiwemo upasuaji wa mfumo wa mkojo, mifupa, uzazi, pua, masikio na koo pamoja na upasuaji wa jumla.

Dk. Shemu amefafanua kuwa serikali ilitoa ajira mpya kwa wafanyakazi 149 wa kada mbalimbali, wakiwemo wa sekta ya afya, ambapo wafanyakazi 16 walipata nafasi ya kushiriki mafunzo ya muda mrefu kwa lengo la kuongeza ujuzi wao.

Amesema kwa sasa hospitali hupokea wagonjwa kati ya 500 hadi 600 kwa siku ikilinganishwa na wagonjwa 200 hadi 300 hapo awali, hatua iliyochangiwa na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa chumba kipya cha upasuaji, uwekaji wa vifaa tiba muhimu katika huduma za dharura pamoja na uwepo wa wodi binafsi.

Ameongeza kuwa hospitali hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa sita litakalojumuisha huduma zote zilizopo ikiwemo huduma maalum za uchunguzi wa afya kwa wanamichezo. “Kabla ya wanamichezo kuanza mashindano tutakuwa tunawapima afya zao. Endapo wakipata changamoto uwanjani watapatiwa huduma hapa hospitalini. Lengo letu ni kuhakikisha wanakuwa na afya njema wanaposhiriki michezo,” amesema.

Akizungumzia hali ya shinikizo la damu, Dk. Shemu amesema takwimu zinaonesha ugonjwa huo husababisha vifo kwa asilimia 50 duniani. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, tafiti zinaonesha kuwa kati ya watu 10 walioko mijini, watu wanne hadi sita wana shinikizo la damu, huku vijijini watu watatu hadi wanne kati ya 10 wakikabiliwa na tatizo hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button