JKCI yazidi kuokoa mamilioni

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa zaidi ya Sh milioni 180 ambazo zingetumiwa na serikali iwapo ingewapeleka wagonjwa 12 wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo kutibiwa nje ya nchi.

Wagonjwa hao waliokuwa na tatizo la uzalishaji wa umeme wa moyo kwa muda mrefu uliosababisha chemba mbili za mioyo yao kufanya kazi bila mawasiliano, wametibiwa katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa na Chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo Cairo, Misri.

Akizungumza kuhusu kambi hiyo ya siku mbili iliyomalizika jana mkoani Dar es Salaam, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa JKCI, Yona Gandye alisema gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa hapa nchini ni Sh milioni 18 lakini nje ya nchi ni zaidi ya Sh milioni 30.

Dk Gandye alisema hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo inaweza kusababisha damu kuganda na kupelekea mgonjwa kupata kiharusi ama kifo cha ghafla kutokana na kiharusi.

Alisema wagonjwa wenye matatizo ya moyo ambayo ni moyo kushindwa kufanya kazi, matatizo ya shinikizo la damu na mshtuko wa moyo, mfumo wao wa umeme wa moyo mara nyingi unaweza kuvurugika.

“Mfumo wa umeme wa moyo ukivurugika utendaji kazi wa moyo hupunguza uwezo wa kufanya kazi na unahitaji kufanyiwa marekebisho ambayo yatauwezesha moyo kuongeza ufanisi wake na kusukuma damu kwa kiwango kinachostahili,” alisema.

Dk Gandye alisema kupitia wataalamu kutoka nchini Misri wataalamu wa JKCI wamepata uwezo wa kufanya matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo kwa kujitegemea, kujenga uhusiano katika kutoa huduma hizo, pamoja na kupanua wigo na uwezo wa ndani wa kuwahudumia Watanzania.

“Hapo awali huduma hii ilikuwa ikitolewa nje ya Tanzania, baada ya serikali yetu kuanzisha taasisi hii na kufunga mtambo maalumu unaoweza kusoma na kutambua matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo Watanzania wameweza kupata huduma hizi hapa nchini.

“Moyo una uwezo wa kutengeneza mapigo yake ambayo huanza kama msisimko na kusambaa ndani ya misuli ya moyo hivyo kuufanya moyo kutanuka na kusinyaa,” alisema.

Dk Gandye alisema magonjwa ya moyo kuna wakati yanaweza kuwepo ndani ya mwili bila kuonesha dalili yoyote hivyo kumfanya mgonjwa kutokutafuta huduma za afya.

“Wananchi tunawahamasisha wawe wanafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kutambua matatizo mapema kwa kufanya hivyo kutarahisisha huduma kuwa nyepesi kufanyika, kupona haraka, na kupunguza madhara makubwa yanayotokana na uchelewaji wa kupata huduma kwa wakati,” alisema.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Hospitali ya Shifa na Chuo Kikuu cha Ain Shams kilichopo Cairo nchini Misri, Profesa Mervat Aboulmaaty alisema hii ni mara yao ya sita kufanya kambi hiyo na madaktari wa JKCI na kuwa mafanikio makubwa yameonekana katika kutoa huduma hizo kwa wagonjwa.

Profesa Mervat alisema wamekuwa wakifanya matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wenye hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuwaachia utaalamu huo wataalamu wa JKCI hivyo kuongeza ubingwa katika kutoa matibabu hayo hapa nchini.

“Kupitia utaalamu tunaobadilishana hapa JKCI, naamini taasisi hii inaenda kuwa taasisi bora zaidi ya kutoa huduma za matibabu ya moyo Afrika Mashariki kwani sisi ni Waafrika hivyo tunapaswa kusaidiana pale tunapohitajiana,” alisema Profesa Mervat.

Hii sio mara ya kwanza kwa JKCI kuokoa mamilioni ya fedha kwa kutibu Watanzania hapa nchini. Mfano ilishawahi kuokoa kiasi cha Sh milioni 580 fedha ambazo serikali ingezitumia kwa kuwapeleka wagonjwa wa moyo 20 nchini India kwa ajili ya matibabu ambapo kwa kila mgonjwa angegharamiwa kiasi cha Sh milioni 29.

Katika taarifa yake ya mwaka 2017 taasisi hiyo ilieleza kufanikiwa kuokoa Sh bilioni 29 kwa kutibu wagonjwa 800 nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button