Job amuomba radhi ‘Morocco’, Watanzania

Dickson Job

DAR ES SALAAM – BEKI wa Yanga, Dickson Job amemwomba radhi Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Morocco amekuwa akimwacha Job kwenye kikosi chake tangu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) iliyofanyika Ivory Coast Januari mpaka Februari kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Morocco alisema wakiwa kwenye mashindano hayo Job aligoma kucheza nafasi ya beki wa kulia kitu alichokitafsiri kama kukosa uzalendo kwa nahodha huyo msaidizi wa Yanga.

Advertisement

Kupitia East Africa Redio, Job alikanusha madai hayo yaliyomfanya kuwekwa kando kwenye kikosi cha Taifa Stars na kocha huyo wa zamani wa Namungo na Geita Gold na kusema yeye ni mzalendo na amezitumikia timu zote za taifa katika umri tofauti.

Hata hivyo, beki huyo wa kati anayetumia akili nyingi uwanjani alisema anaamua kumwomba radhi kocha huyo pamoja na Watanzania waliokwazika na madai hayo ya kwamba hana uzalendo kwa taifa lake.

“Sijawahi kugomea majukumu ya kocha lakini yeye ni kocha wangu hivyo namwomba radhi pamoja na Watanzania kwani najua walikwazika baada ya kusikia mimi siyo mzalendo,” alisema Job.

SOMA: Miquissone, Chilunda ‘bye bye’ Simba

Job ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani na wakiwa kwenye mashindano ya Afcon kwa mujibu wa Morocco alimtaka beki huyo wa Yanga kucheza nafasi ya beki wa kulia kitu ambacho alikigomea akitaka kupangwa nafasi ya mlinzi wa kati aliyoizoea.