Kabudi: Vyama vitumie fursa ya mazungumzo

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amevitaka vyama vya siasa kutumia fursa ya mazungumzo, ambapo amesema milango ya Serikali iko wazi na Rais Samia Suluhu Hassan yupo tayari kuwasikiliza wasiwe na hofu.
Prof Kabudi amesema hayo leo, Oktoba 7, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Uongozi Mpya na Nembo ya Baraza la Vyama vya Siasa, hafla iliyohudhuriwa na wawakilishi wa vyama mbalimbali, akiwemo NCCR Mageuzi, TLP, CUF, NRA, DP, CCK, AFP, ACT Wazalendo, UDP, SAU, ADC, TLS na CHAUMA.
Amesema Rais Samia amesisitiza umuhimu wa viongozi wa vyama kukaa pamoja na kujadiliana, akieleza kuwa Serikali iko tayari kupokea maoni yao kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa au Baraza la Vyama vya Siasa,
“Dk Samia Suluhu Hassan amesisitiza tukae pamoja tuzungumze, na mimi naomba tukae pamoja tuzungumze, mlango wa serikali uko wazi njooni tuzungumze kwa kupitia msajili ama Baraza la Vyama vya Siasa, lakini mnapokuja kuzungumza pia ukubali lazima kuwe na muafaka sio lazima unalolitaka lipitishwe” amesema Prof Kabudi.
Aidha, amesema maoni yanapaswa kutolewa kwa lugha ya staha, kiungwana na kwa heshima, huku akiwataka kuepuka lugha ya matusi.
Aidha, Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa kuheshimu wanawake katika siasa, kuimarisha uwajibikaji na kuendelea kupambana na rushwa, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kujenga mazingira bora ya kisiasa na kuimarisha demokrasia nchini.



