KAGAME: Rwanda haihusiki kuifadhili M23

RWANDA : RAIS wa Rwanda, Paul Kagame, amesisitiza kuwa serikali ya Rwanda haitoi msaada kwa wapiganaji wa kundi la M23 wanaosababisha ghasia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kama inavyodaiwa.

Akizungumza kuhusu vita vinavyoendelea katika eneo hilo kwa miaka mingi, Rais Kagame alikosoa madai ya kwamba Rwanda inahusika, akisema: “Je, watu hapa hawajui jinsi vita hivi vilivyoanza? Vita hivi vilianza miaka mingi iliyopita na haikutokana na Rwanda.”

Aliongeza kuwa, ingawa baadhi ya makundi ya waasi yana asili ya Rwanda, walihamia Congo tangu enzi za ukoloni na walikuwa na mizizi ya kihistoria katika eneo hilo.

Advertisement

Rais Kagame alisisitiza kuwa ingawa viongozi wa Congo wamesema waasi hao ni Wakongo, bado wanadai kuwa Rwanda inahusika katika vita hii, jambo ambalo amelipinga.

Alifafanua kuwa waasi hao wanatokana na makundi ya zamani yaliyokuwepo huko kabla ya vita hivi, na kwamba hakuna msaada wowote kutoka Rwanda.

Kauli ya Rais Kagame inakuja baada ya kundi la M23 kuchukua udhibiti wa mji wa Masisi mashariki mwa DRC. SOMA: Rwanda Congo wakubaliana kumaliza mivutano

Wakosoaji wa Rwanda wanaishutumu nchi hiyo kutumia kundi la M23 kutafuta madini  kutoka DRC, ikiwa ni pamoja na dhahabu, cobalt, na tantalum, ambayo hutumika kutengeneza bidhaa za kiteknolojia kama simu za mkononi na betri za magari ya umeme.

Mwezi uliopita, DRC iliipeleka Apple mahakamani kwa matumizi ya “madini ya damu,” huku kampuni kubwa ya teknolojia ikitangaza kwamba imeacha kununua madini kutoka kwa nchi hizo mbili.

Hata hivyo, Rwanda imekanusha madai hayo na kudai kuwa haitumii madini kutoka DRC kwa njia haramu.