Kairuki ataka ulinzi nyanzo vya maji

MOROGORO: WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema bila majisafi na salama jamii haiwezi kustawi, uchumi hauwezi kukua na mazingira hayawezi kuendelea.

Kufuatia umuhimu huo jamii inalo jukumu kubwa la utayari kwa kila mmoja kuhakisha nawajibika kulinda vyanzo vya maji na uhifadhi mazingira.

Waziri Kairuki alitoa wito huo mjini Morogoro kwenye ufunguzi wa Mdahalo wa Wadau kuhusu Maji na Jinsia ulioandaliwa na Wizara ya Maji ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Maji.

Wizara ya Maji inaadhimisha Wiki ya Maji ambayo inaanza Machi 16, hadi 22 Machi ambayo ni Siku ya Maji Duniani.

Amesema jamii ina wajibu kushughulikia masuala ya maji na jinsia kwa pamoja ili kufungua njia za uwezeshaji, usawa, na maendeleo endelevu katika upangaji na utekelezaji wa miradi na sera ya Sekta ya Maji.

Waziri huyo amesema kuwa maji yanatunza mazingira pamoja na kaya, yanasaidia kilimo, yanabeba viwanda.

Amesema kuwa Serikali imetambua umuhimu wa maji na kufanya kuwa moja ya agenda za vipaumbele muhimu katika jitihada za kuboresha maisha ya wananchi.

Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati na kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema kuwa Wizara ya Maji imejipanga kuhakikisha inatoa majibu ya changamoto zote zinazowakumba wananchi kwa jinsia zote katika upatikanaji wa majisafi na salama.

Mhandisi Waziri amesema Wizara ya Maji inatambua kuwa changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama bado inaathiri makundi mbalimbali katika jamii kwa namna tofauti, hususan wanawake na wasichana ambao hubeba jukumu kubwa la kutafuta na kusimamia matumizi ya maji katika ngazi ya familia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Jackson Kiswaga amesema kamati anayoiogoza ipo tayari kupokea mawazo ya wadau na kuyafanyia kazi.

“Kazi kubwa ya Bunge ni kutunga Sheria, kuisimamia Serikali, na kuwawakilisha wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania,” amesema Kiswaga.

Kiswaga amesema ni matumaini yao kupitia Mdahalo huo yatapatikana mapendekezo kuhusu maeneo muhimu ya kuzingatia wakati wa utungaji wa sheria ili kuhakikisha kuwa masuala ya kijinsia yanazingatiwa ipasavyo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la WaterAids, Christina Mhando, amesema shirika hilo linaamini maji si tu huduma bali ni njia ya kufungua milango ya usawa wa kijinsia katika jamii.

Amesema jamii zinazopata huduma bora ya maji, wanawake na wasichana ambao hubeba mzigo mkubwa na linapokuja suala la upatikanaji wa maji maisha yao hubadilika na wanapata afya bora, muda na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button